NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) zimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano yenye lengo la kuimarisha utendaji, kurahisisha mzunguko wa bidhaa na kuboresha usimamizi wa viwango katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makubaliano hayo, ambayo ni ya tatu kati ya taasisi hizo mbili, yataanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2025 hadi 2030.
Akizungumza katika hafla hiyo leo Septemba 4, 2025 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), David Ndibalema amesema kuwa ushirikiano kati ya TBS na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) umeendelea kuimarika na umeleta mafanikio makubwa katika kurahisisha biashara na kulinda usalama wa watumiaji wa bidhaa katika pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kuwa TBS ni taasisi kongwe ambayo mwaka huu inatimiza miaka 50 ya utoaji huduma za viwango na ubora, wakati ZBS ilianzishwa baadaye, hivyo kuna umuhimu wa kushirikiana ili kubadilishana uzoefu na uwezo, hasa katika sekta ya maabara na usimamizi wa viwango.
“Ili biashara ifanyike vizuri, ni lazima viwango vioanishwe. Hii inahakikisha bidhaa zikivuka upande mmoja kwenda mwingine zinakubalika kwa urahisi na usalama wa wananchi unalindwa,” amesema Ndibalema.
Ameongeza kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, sambamba na kuboresha afya na ustawi wa Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yusuph Majid Nassor amesema ushirikiano huo umekuwa chachu ya maendeleo, hususani katika kujengewa uwezo na uimarishaji wa maabara.
“TBS ina historia ya miaka 50, wakati ZBS tuna miaka 15 tu tangu kuanzishwa mwaka 2011. Ushirikiano huu ni msingi muhimu wa maendeleo yetu,” amesema Nassor.
Aidha amesema kuwa awali bidhaa kutoka upande mmoja zilikuwa zikikumbwa na vikwazo katika kuingia upande mwingine, lakini kupitia makubaliano haya, changamoto hizo zimepatiwa suluhisho.
“Leo bidhaa yoyote yenye alama ya ubora ya TBS au ZBS inaruhusiwa kuingia bila kizuizi chochote. Maji yanayozalishwa Bara yanaingia Zanzibar na bidhaa kutoka Zanzibar zinaingia Bara bila matatizo,” ameongeza Nassor.