Ukara, Ukerewe
Wakazi wa Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wameishukuru Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa hatua ya kuanza kuzikarabati baadhi ya barabara za kisiwa hicho, ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zinapitika kwa shida.
Wakizungumza wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, wamesema kwa sasa barabara hizo zinapitika bila adha yoyote baada ya TARURA kuzikarabati kwa kiwango cha changarawe.
Aidha, wameomba TARURA kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka darajani kuelekea hospitali ya Bwisya.
Kilio cha wakazi wa kisiwa cha Ukara, kinafuatia ahadi za viongozi wakuu wa kitaifa ambao kwa nyakati tofauti wametembelea kisiwa hicho na kuahidi kujenga barabara za Nyamanga-Bwisya, Katende-Bugaramila na Bwisya-Kome zenye jumla ya urefu wa Km 2 kwa kiwango cha lami, ambapo upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hizo tayari umeshafanyika.