Zanzibar – Chama cha Wataalamu wa Misitu Tanzania (TAF) kimetakiwa kujadili njia mpya za kulinda misitu kwa kutumia maarifa ya kisayansi na teknolojia za kisasa ili kukabiliana na changamoto za ongezeko la watu na ukataji miti ovyo.
Wito huo umetolewa leo Septemba 4, 2025 na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar, Mhe. Shamata Shaame Khamis, wakati akifungua Mkutano wa 21 wa chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Zanzibar.
Amesema misitu ni nguzo muhimu kwa maisha ya viumbe vyote, lakini kwa sasa inakabiliwa na vitisho vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wa vizazi vijavyo na kufifisha juhudi za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu endapo haitalindwa kwa mbinu za kisasa.
“TAF inapaswa kuwa daraja kati ya wataalamu, serikali, sekta binafsi na jamii ili majadiliano ya pande zote yahakikishe matokeo chanya kwa sekta ya misitu,” amesema Waziri Khamis.
Aidha, amesema serikali zina matumaini makubwa kupitia chama hicho, kwani kina jukumu la kuwaunganisha wadau mbalimbali na kuchochea uhifadhi endelevu wa misitu, jambo linalohusiana moja kwa moja na vipaumbele vya uchumi wa buluu, nishati safi na hifadhi ya mazingira.
Kwa upande wake, Rais wa TAF, Joseph Stiima Makeko, amesema chama hicho kiko tayari kushirikiana na wadau kuhamasisha uhifadhi wa misitu na vyanzo vyake kwa lengo la kulinda rasilimali na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.