NA JOHN BUKUKU- NJOMBE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imeanza mchakato wa ujenzi wa uwanja mpya wa ndege mkoani Njombe ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara, hususan parachichi na chai, kwenda sokoni.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni, Dkt. Samia amesema ili kuhakikisha mapinduzi makubwa yanafanyika kwenye kilimo, serikali itajenga vituo 50 vya kuhifadhia matunda, kuajiri maafisa ugani maalumu kwa ajili ya zao la parachichi pamoja na kuweka ruzuku kwenye dawa na mbolea za kikorganic kwa zao hilo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia ameeleza kuwa serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Itoni–Manda ili kurahisisha usafirishaji wa malighafi za madini. Aidha, amebainisha kuwa hivi karibuni shughuli za uchimbaji wa madini ya Liganga na Mchuchuma zitaanza rasmi.
Awali, wakieleza mahitaji ya wakazi wa majimbo ya Njombe, wagombea ubunge akiwemo Deo Mwanyika (Njombe Mjini), Rebecca Nsemwa (Viti Maalumu), Joseph Kamonga (Ludewa) na Edwin Swalle (Lupembe) walisema licha ya serikali ya Mama Samia kufanya mambo makubwa katika miradi ya maendeleo hususan maji, umeme, afya na kilimo, changamoto ya barabara na kuyumba kwa zao la chai zinahitaji jitihada za ziada kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo.
Kwa upande wao, wakazi wa Njombe akiwemo Edger Mtitu na Dkt. Cholastica Kevela, ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Njombe, wamesema ifikapo Oktoba 29 watakwenda kumzawadia kura za kutosha Rais, wabunge na madiwani wa CCM kutokana na kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Wameomba pia sekta za elimu, maji na barabara zipewe kipaumbele zaidi.