Tandahimba, Septemba 4, 2025
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Tandahimba imekabidhi kiasi cha shilingi 500,000/= kwa Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Salama, Mwl. Mustafa Shaibu Rashidi, fedha zilizookolewa kufuatia malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Mkupete (W) Tandahimba.
Malalamiko hayo yalitolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Aprili, 2025, ambapo wananchi walieleza kuwa walichanga fedha kwa ajili ya kumlipa mwalimu wa somo la Biology na Elimu ya Dini ya Kiislam katika Shule ya Sekondari Salama. Hata hivyo, Mwl. Lameck Sijaona Kijalo, aliyekuwa akisimamia michango hiyo, alituhumiwa kuzitumia fedha hizo kwa manufaa yake binafsi.
Fedha hizo zilikabidhiwa rasmi leo na Afisa wa TAKUKURU Wilaya ya Tandahimba, Bi. Siudhiki Mohamed Joginda, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, mbele ya wananchi wa Kijiji cha Mkupete.
TAKUKURU imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha mali za umma na michango ya wananchi inalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.