Wahitimu wa darasa la saba shuleni hapo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mahafali hayo.
Mmoja wa wanafunzi aliyehitimu darasa la saba akikabithiwa cheti katika mahafali hayo.
……………..
Happy Lazaro, Arusha
Wahitimu wa darasa la saba wametakiwa kujiendeleza zaidi pamoja na kujiepusha na makundi yasiyofaa kwani safari yao ya maisha ndo imeanza.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mraribu wa nchi katika shirika lisilo la kiserikali la Sopowerful Foundation Angel Mollel wakati akizungumza na wazazi pamoja na wanafunzi wa shule ya mchepuo wa kiingireza ya Bethlehem Star Pre&Primary katika mahafali ya 6 ya darasa la saba katika shule hiyo ambapo jumla ya wanafunzi 32 walihitimu.
Mollel amesema kuwa, wanafunzi hao wanatakiwa kutambua kuwa hapo ndo bado safari imeanza hivyo ni jukumu lao kuwa na motisha ya kujiendeleza zaidi ikiwa ni pamoja na kujiepusha na makundi mbalimbali yasiyofaa ambayo mwisho wa siku yanawaharibia malengo yao.
Ameongeza kuwa, shirika hilo limeweza kuwafungia sola shuleni hapo kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kupata umeme muda wote pindi umeme unapokuwa hakuna na kuweza kujisomea muda wowote, ambapo mbali na mashuleni pia wamekuwa wakifunga kwenye hospitali.
“Tumekuwa tukisaidia jamii ya mazingira magumu hasa mashuleni hivyo tunatoa wito kwa shule zote tulizofunga kuhakikisha wanatunza ili ziweze kutumika kwa vizazi vijavyo.”amesema.
Kwa upande wake Meneja wa shule hiyo ,Christina Lyimo amesema kuwa ,shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri sana katika taaluma kutokana na walimu waliobobea ambao wamekuwa wakifundisha wanafunzi hao kwa vitendo zaidi.
Lyimo amesema kuwa ,kwa miaka yote mfululizo tangu kuanzishwa kwa shule hiyo wanafunzi hao wamekuwa wakiongoza katika masomo yao kwa kuwa vinara.
Amefafanua kuwa, wanafunzi hao wamekuwa wakijiamini katika kufanya maswala mbalimbali na hiyo ni kutokana na ubora wa walimu uliopo ambao wamekuwa wakiwaandaa wanafunzi hao kujiamini wakiwa tangu wadogo.
“Nawaombeni sana wanafunzi pindi mnapohitimu hapa mhakikishe yale yote mliyoyapata hapa mnayaendeleza pamoja na kutanguliza nidhamu mbele kwani huu ndo mwanzo tu na safari ndo imeanza.”amesema Lyimo.
Aidha amewataka wazazi kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao ili waweze kujua changamoto zinazowakabili pamoja na kutoa motisha kwao ili waendelee kufanya vizuri zaidi.
Kwa upande wa wanafunzi waliohitimu masomo yao wanashukuru shule hiyo kwa namna ambavyo imeweza kuwaandaa kujiamini katika kila wanachokifanya sambamba na kuwafundisha kujiajiri kwa kujifunza masomo mbalimbali ya ujasiriamali.