NA JOHN BUKUKU- IRINGA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya. Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga soko la machinga na kueleza kuwa eneo tayari limeshatengwa na sasa taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga Machinga Complex ndani ya Mkoa wa Iringa zimeanza.
Ameyasema hayo leo wakati akihutubia mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Samora, Iringa Mjini.
“Nataka nimalize Machinga Complex ndani ya mkoa wa Iringa ili machinga na mama lishe wote waweze kufanya biashara zao,” amesema Samia.
Amefafanua zaidi kuwa, Manispaa imetenga ofisi ya machinga mkoa na atatoa fedha kujenga ofisi za machinga katika mikoa yote nchini ambazo zitarahisisha uratibu wa shughuli zao.
Amesema kuwa, alipofanya ziara ndani ya mkoa huu Agosti 2022, pamoja na mambo mengine aliahidi mambo kadhaa ikiwemo kuleta scheme za umwagiliaji. Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya umwagiliaji maji ikiwemo miradi tisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa zaidi ya shilingi bilioni 529, mradi huo umewezesha shughuli za kilimo kuendelea kwa muda wote.
Amesema kuwa, hayo yote yanalenga kuwezesha wakulima kuendelea na kilimo.
Serikali iliendelea kutoa pembejeo na mbolea kwa ruzuku ambayo imewezesha wakulima kuzalisha kwa wingi.
“Nilitolea mfano hapa Iringa, zao la kahawa uzalishaji umeongezeka kutoka tani 109 mwaka 2020 hadi kufikia tani 323 mwaka huu,” amesema.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa Mbarali mpunga upo kila mahali na wameweza kukuza uzalishaji wa mazao. Kwa upande wa mahindi, kutokana na pembejeo na mbolea ya ruzuku, mwaka huu Tanzania imekuwa ya pili kwa uzalishaji wa mahindi Afrika baada ya kuzalisha tani milioni 10. Hivyo, mbolea na pembejeo za ruzuku zimekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kilimo.
“Hivyo basi, mkitupa ridhaa tutaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kote nchini pamoja na pembejeo,” amesema.
Aidha, amesema kuwa watajenga vituo 50 vya kuhifadhia mazao ya parachichi, vituo vingine vya kuhifadhia mazao ya mboga mboga, na pia maghala kwa ajili ya kuhifadhia mazao ya chakula na biashara.
Amefafanua kuwa wataanzia kwenye vituo vya zana za kilimo ili wakulima waweze kunufaika kwa bei nafuu kwani vituo hivyo vitatoa huduma kwa nusu ya bei.
Akizungumzia upande wa nishati, amesema kuwa aliahidi kufikisha umeme kwenye vijiji vyote 360 vya Mkoa wa Iringa, na kazi inayoendelea sasa ni kupeleka umeme kwenye vitongoji ambapo vingi tayari vimepata.
“Kwa hapa Iringa Mjini tumefikisha umeme kwenye mitaa yote 186 kati ya 192, vichache vilivyobaki kazi inaendelea,” amesema.
“Pamoja na kusambaza umeme Tanzania nzima mijini, vijijini na vitongoji, tuna kazi ya kuendesha uzalishaji wa umeme wenyewe ili uweze kutosha. Tumetoka megawati 1,600 mwaka 2020 na mpaka mwaka huu tuko megawati 4,000, na sasa tunajipanga kufikisha megawati 8,000 kwa kutumia vyanzo mbalimbali. Hivyo tunajipanga vyema ili umeme uwe msingi na kichocheo cha maendeleo ya nchi yetu,” amesema.
Amefafanua kuwa kuanzishwa kwa Kiwanda cha Ndege cha Nguli kumeanza kutoa matunda, ambapo mashirika kadhaa ikiwemo Air Tanzania tayari yameanza kutoa huduma.
“Atahakikisha anashughulikia barabara zote na madaraja ambayo hayajakamilika endapo watapewa ridhaa,” amesema.
Akizungumzia sekta ya miundombinu, amesema amepokea maombi mengi ndani ya mkoa huu kuhusu barabara ambapo ujenzi wa kilometa moja ya barabara ya lami unagharimu zaidi ya shilingi bilioni moja. Serikali itaendelea kujenga barabara mbalimbali za kokoto ili ziweze kupitika muda wote na pia itafungua barabara nyingine mpya.
“Mbali na hayo, tumechukua hatua mbalimbali kuwezesha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji. Tumefanya kazi nzuri sana katika kipindi cha miaka minne hadi mitano iliyopita,” amesema.
“Katika kukuza uchumi na ajira kwa vijana, mkoa wa Iringa umewekeza kwenye viwanda. Wakati naingia madarakani, mkoa huu ulikuwa na viwanda vikubwa 24 na sasa kuna viwanda 40, hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana wetu. Mkitupa ridhaa, tumejipanga kuanzisha na kuboresha viwanda katika wilaya zote za Tanzania ili tuongeze uwekezaji na thamani ya mazao yetu kwa wananchi,” ameongeza.