NA JOHN BUKUKU- IRINGA
MGOMBEA Kiti cha Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema hatua zilizochukuliwa na serikali yake zimeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa mahindi, jambo linalodhihirisha ukuaji wa sekta ya kilimo na mchango wake katika uchumi wa taifa.
Akizungumza kwenye kampeni za Uwanja wa CCM Samora mkoani Iringa, Dk. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema serikali imekamilisha skimu ya umwagiliaji yenye thamani ya Sh. Bil. 104.4 mkoani humo, ikinufaisha zaidi ya wakulima 62,800 na kuongeza tija ya kilimo. Alibainisha kuwa mafanikio hayo yamechangia ongezeko la uzalishaji wa mahindi kufikia tani Mil. 10 mwaka huu.
“Nilipofanya ziara ndani ya mkoa huu mwezi wa nane mwaka 2022 pamoja na mambo mengine niliahidi mambo yafuatayo, nimeahidi nitaleta skimu za umwagiliaji maji,” alisema Dk. Samia.
Aidha, alisema katika sekta ya kahawa, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 109 mwaka 2021 hadi tani 323 mwaka huu, ongezeko linalowapa wakulima kipato na matumaini mapya.
“Lakini jana nilizunguka kule Mbalali, nikaenda Mwakalenga nikawasikiliza wabunge wa Mbarali, nimeona mwenyewe mipunga kotekote, kwa hiyo mashine zile za kukata mpunga kote kote zimejaa,” alisema.
Katika upande wa nishati, Rais Samia alisema uzalishaji wa umeme umeongezeka kutoka megawati 1,600 mwaka 2021 hadi megawati 5,000 mwaka huu, huku lengo likiwa kufikia megawati 8,000 ili kuchochea viwanda na ajira.