Na Mwandishi Wetu
HOSPITALI ya Mfumo wa Mkojo na Uzazi ya MDM ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam imeandaa kambi maalum endelevu kuanzia tarehe 8 Jumatatu kwaajili ya matibabu ya maradhi ya mfumo wa mkojo na mfumo wa uzazi.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Dk Mathias Kimolo ambaye ni daktari bingwa mbobezi wa mfumo wa mkojo katika hospitali hiyo ya MDM Urology.
Alisema lengo kuu la kuandaa kambi hiyo endelevu ni kuvunja ukimya kwenye jamii kwamba magonjwa hayo yapo na yanatibika kwakuwa magonjwa ya mfumo wa uzazi yanafichwa na watu wengi kwenye jamii.
“Tunawaasa wenye magonjwa hayo kufika hospitalini kwetu watapata vipimo na watakaokutwa na shida watapatiwa matibabu stahili kwa hiyo tunawakaribisha watu wote,” alisema
“Magonjwa mengine tunayolenga kuyatibu ni upungufu wa nguvu za kiume kwa wanaume kushindwa kusimamisha uume, ugonjwa huu unafanywa siri lakini umeathiri wanaume wengi waliovuka miaka 40,” alisema
Alisema tatizo linaweza likawa kubwa zaidi kwani takwimu zinazotolea ni kwa wale tu ambao wamekwenda hospitani na kundi kubwa bado halijaenda kupata matibabu.
“Kuna utafiti ulifanyika wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro mwaka 2020 ambao ulionyesha kuwa kati ya wanaume watatu mmoja anashida kwenye nguvu za kiume na mwingine ulifanyika hapo hapo Moshi mwaka 2023 ukaonyesha kuwa wanaume wanaoishi na VVU walionekana wanashida kubwa ya nguvu za kiume,” alisema na kuongeza
“Utafiti ulionyesha kuwa wenye VVU wanashida mara mbili ya wale ambao hawana VVU na wanaume watatu kati ya wanne wenye VVU wanashida ya nguvu za kiume,” alisema
“Hili tatizo lipo ila linafanywa siri sasa sisi tunataka kuieleza jamii kwamba tatizo linaweza kutibika na matibabu ya aina mbalimbali kuanzia dawa, ushauri na upasuaji na matibabu mengine baada ya kupima na kugundua tatizo,” alisema.
Alisema tatizo lingine ambalo wataliangalia kwenye kambi hiyo ni kuwa na mawe kwenye mfumo wa mkojo na ambao ni ugonjwa unaosumbua kwenye nchi nyingi za Afrika Mashariki.
Alitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kupata maumivu kwenye mbavu yanayobana na kuachia, shida kwenye mkojo kwa mhusika kukojoa mara kwa mara kutokana na mawe yaliyoko kwenye njia ya mkojo.
“Tuna aina mbalimbali ya matibabu kulingana na ukubwa wa jiwe na sehemu ambayo hilo jiwe lipo, kama liko kwenye figo tunaweza kutibu bila kufanya upasuaji kwa mgonjwa. Tunatumia mawimbi mtetemo inayovunja mawe kwenye figo na mgonjwa anayakojoa kwa kuwa yanakuwa yamesagika sagika,” alisema
Alisema tatizo lingine watakalotibu ni tezi dume ambayo huwaathiri wanaumewengi kuanzia miaka 50 ambapo tezi dume huvimba na kuzuia njia ya mkojo.
“Matibabu haya pia yako ya aina mbalimbali, baada ya vipimo mhusika anaweza kupatiwa matibabu ya dawa au kufanyiwa upasuaji wa ndani kwa ndani bila kupasua nje na kama mambo yamekwenda vizuri mgonjwa anaweza kukaa hospitali siku mbili na kuruhusiwa kwenda nyumbani,” alisema
Alisema ugonjwa mwingine watakaotibu ni makovu ya kwenye njia ya mkojo ambayo yanasababisha mkojo kutoka kwa kusuasua na kwamba hiyo uzoefu unaonyesha kuwa wengi wanaoathiriwa na hali hiyo ni wale waliowahi kupata magonjwa ya gono.