Algiers, Algeria – Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeibuka kinara katika kutangaza bidhaa za misitu na nyuki kupitia maonesho ya kimataifa ya biashara barani Afrika (Intra African Trade Fair – IATF 2025) yanayofanyika jijini Algiers, Algeria, yakihusisha nchi zaidi ya 33.
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Imani Njalikai, alisema Algeria ina uhaba mkubwa wa mazao ya misitu, hali inayotoa fursa kwa Tanzania kupeleka mbao na mazao mengine.
“Nchi ya Algeria ina misitu michache kwa uzalishaji wa mazao ya misitu. Tunahitaji mbao hapa; wekeni utaratibu maalumu wa kufikisha bidhaa zenu ili tutangaze fursa hizi,” alisema Balozi Njalikai.
Kwa mujibu wa TFS, kupitia kampuni tanzu yake ya Misitu Company, taasisi hiyo inashiriki vikao vya biashara kwa njia ya B2B, makongamano ya uwekezaji na majukwaa ya majadiliano, ikitangaza bidhaa kuu zikiwemo mbao za mtiki na pinus spp, pamoja na asali ya msitu inayojulikana kwa ubora wa kimataifa.
Aidha, TFS imeweka mkakati wa kutumia maonesho hayo si tu kuuza bidhaa, bali pia kuvutia wawekezaji na washirika wa kimkakati watakaochangia kuimarisha biashara endelevu ya mazao ya misitu na nyuki nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kampuni ya Misitu, Grace Buchukundi, alisema kampuni hiyo inalenga kujenga mahusiano ili kuongeza thamani ya mazao ya misitu kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa kimataifa.
Maonesho ya IATF 2025, yanayoendelea hadi Septemba 10 , yamewaleta pamoja viongozi wakuu wa nchi, wawekezaji na taasisi mbalimbali za Afrika. Tanzania inawakilishwa na taasisi kadhaa zikiwemo TANTRADE, TMDA, NEMC, FCC, TISEZA, PURA na ZIPA, huku Wizara ya Viwanda na Biashara ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Suleiman Hassan Serera.
Kwa mujibu wa ratiba, washiriki wanatarajiwa kushuhudia fursa mpya kupitia mikutano ya uwekezaji, mijadala ya AfCFTA na majukwaa ya sekta za kilimo, nishati na biashara za kidigitali – hatua inayotajwa kuwa kichocheo cha mabadiliko ya biashara barani Afrika.