Columbia Africa Healthcare Limited imetangaza ununuzi wa IST Clinic, kituo maarufu cha huduma za afya kilichopo Dar es Salaam. Kupitia ununuzi huu wa hisa kwa asilimia 100, Columbia Africa inaimarisha uwepo wake katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ikiongeza Tanzania kwenye mtandao wake wa kliniki uliopo Nairobi, Kenya.
Ununuzi huu ni hatua muhimu katika mkakati wa Columbia Africa wa kupanua huduma bora, nafuu na zinazomlenga mgonjwa katika Afrika Mashariki. Baada ya mchakato wa muunganiko, IST Clinic itafanya kazi chini ya jina la Columbia Africa.
Kama sehemu ya dhamira yake ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini Tanzania, wagonjwa wa IST Clinic wataendelea kupata huduma bila usumbufu, wakiendelea kuhudumiwa na timu ile ile ya madaktari waliowazoea, huku wakiwa sasa wanapata msaada wa utaalamu wa kimataifa kutoka Columbia Africa.
Muunganiko huu utafanya maboresho yafuatayo: Ubora wa Juu wa Huduma – kupitia utambulisho wa mifumo ya kitabibu yenye viwango vya kimataifa na kanuni za usalama kwa wagonjwa.
“Tunafuraha kubwa kuipokea IST Clinic ndani ya familia ya Columbia Africa. Ununuzi huu si tu hatua ya ukuaji – bali ni ahadi ya kuleta huduma za afya za viwango vya kimataifa karibu na jamii za Tanzania, huku tukiendelea kudumisha mahusiano thabiti ambayo wagonjwa wameyajenga na madaktari wao,” alisema Dkt. Sumit Prasad, Mkurugenzi Mtendaji, Columbia Africa.
Ype Smit, MD, Mwanzilishi na Mkurugenzi, aliongeza: “Kwa zaidi ya miaka 25, IST Clinic imekuwa ikitoa huduma zinazomlenga mgonjwa moja kwa moja jijini Dar es Salaam. Kujiunga na Columbia Africa kunatupa nafasi ya kuunganisha historia hii na mifumo ya kisasa ya kitabibu, teknolojia na viwango vya kimataifa vya huduma ili kuwatumikia wagonjwa wetu kwa ubora zaidi.”
Tangu kuanzishwa mwaka 1997, IST Clinic imekua na kuwa mtoaji wa huduma za afya zenye ubora wa hali ya juu jijini Dar es Salaam, ikitambulika kwa huduma za kibinafsi na endelevu. Kupitia timu yake ya madaktari, wauguzi, maabara na wafamasia, IST Clinic imetumikia vizazi vingi vya familia na kuendelea kuwa mshirika anayeaminika wa afya nchini Tanzania.
Columbia Africa, ikiwa sehemu ya makampuni ya afya ya Columbia Pacific Management, inaleta uzoefu wa miongo kadhaa katika kuendeleza hospitali na vituo vya kutoela huduma za afya barani Asia, Afrika na China. Ujio wake Tanzania unaonesha zaidi dhamira ya kujenga mifumo endelevu ya afya katika maeneo yenye ukuaji wa haraka.
Kuhusu Columbia Africa
Columbia Africa Healthcare Limited ni kampuni binafsi ya huduma za afya yenye makao yake makuu Nairobi, Kenya. Inafadhiliwa na Columbia Pacific Management Inc., kampuni yenye makao yake Seattle, Marekani, yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika kuendeleza huduma za afya na makazi ya wazee duniani. Columbia Africa inatoa tiba inayozingatia uthibitisho wa kisayansi kupitia mazingira ya kisasa, yenye ufanisi na kujali, yaliyobuniwa kukidhi mahitaji ya kiafya ya miji inayoendelea kukua barani Afrika.
Kuhusu IST Clinic
IST Clinic, iliyoanzishwa mwaka 1997, ni mtoa huduma za afya za kila siku iliyopatika katika eneo la Peninsula, Dar es Salaam, Tanzania. Inatambulika kwa huduma zinazomlenga mgonjwa na mwendelezo wa huduma, IST Clinic imejijengea sifa ya tiba ya kibinafsi, ubora wa kitabibu na kuaminika na jamii.