Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Addis (AICC) Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Tarehe 08 Septemba 2025.
…………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema licha ya Afrika kuchangia chini ya asilimia nne katika uzalishaji wa hewa chafu duniani lakini ndiyo inayoathiriwa zaidi na mabadiliko ya Tabianchi na hivyo kuhitaji usaidizi wa haraka katika kuhimili hali hiyo na kuhakikisha mapinduzi ya kijani.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia katika Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia. Ametoa wito kwa washirika wa Kimataifa kutekeleza ahadi zao za utoaji fedha katika njia mpya na zinazotabirika kama ilivyokubaliwa chini ya Mkataba wa Paris na kuendesha Mfuko wa Hasara na Uharibifu kwa rasilimali za kutosha.
Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuzingatia malengo ya Kimataifa ya kuhakikisha hali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi inapewa kipaumbele sawa na hali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema mageuzi katika nishati ni nguzo muhimu katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ameongeza kwamba, Tanzania inaendelea kuongeza uwekezaji katika nishati jadidifu kupitia umeme wa maji, jua, jotoardhi na upepo, huku pia ikitumia gesi asilia kama nishati safi ya mpito kusaidia ujenzi wa viwanda pamoja na kutekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia, unaolenga kuhakikisha asilimia themanini ya kaya zinatumia nishati safi kupikia ifikapo 2034.
Pia, Makamu wa Rais amesema Tanzania inaendelea na dhamira ya kujitolea kufanya kazi na wadau wote ili kuendeleza azma ya kusambaza umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030 kama ilivyodhamiriwa katika Mkutano wa Nishati wa Afrika wa Misheni 300 uliofanyika Dar es Salaam Januari 2025.
Ameongeza kwamba Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar na Mpango Mkakati wa Uchumi wa Buluu kwa upande wa Tanzania Bara, huimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, pwani na nchi kavu, kusaidia ajira na ustahimilivu katika shughuli za uvuvi, usafiri wa baharini na utalii.
Makamu wa Rais amesema Tanzania ikiwa na heshima ya kuwa mwenyekiti wa kundi la majadiliano la Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi (AGN) kuelekea Mkutano wa COP30 nchini Brazil, itaendelea kufanya kazi kwa bidii kuratibu msimamo wa pamoja wa Afrika na kuhakikisha vipaumbele ya bara hilo, fedha, hasara na uharibifu pamoja na mabadiliko ya haki yanazingatiwa katika majadiliano hayo.
Amesema Mkutano wa 30 wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) ili uwe na mafanikio ni lazima utoe matokeo kabambe, jumuishi na yenye usawa. Ameongeza kwamba, Tanzania itatoa usaidizi kamili kwa nchi ya Brazili ili kuhakikisha kuwa mkutano huo unatekelezwa kwa ajili ya Afrika na dunia kwa ujumla.
Makamu wa Rais amesema Tanzania itaendelea kukuza sauti ya Afrika, kutafuta njia, pamoja na kufanyia kazi matokeo yenye maana ambayo yanaakisi mahitaji ya Afrika na uwezo wake kama mshirika katika masuluhisho ya kimataifa.
Kabla ya kuanza kwa Mkutano huo, Wakuu wa Nchi na Serikali waliongoza zoezi la upandaji miti ikiwa ni ishara ya njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kaulimbiu ya Mkutano huo ni “Kuharakisha suluhu za mabadiliko ya tabianchi duniani na ufadhili kwa maendeleo endelevu, yenye ustahimilivu na maendeleo ya kijani barani Afrika (Accelerating Global Climate Solutions and Financing for Africas’ Resilient and Green Development).
Mkutano huo umetanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo Wiki ya Tabianchi ya Afrika kwa mwaka 2025 iliyofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 6 Septemba 2025, kwa lengo la kuendeleza hatua za kuharakisha utekelezaji wa malengo ya Mkataba wa Paris kuhusu tabianchi.
Licha ya wawakilishi wa Serikali, Mikutano hiyo pia imehudhuriwa na vijana, sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe.Hamza Hassan Juma, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Cyprian Luhemeja, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe. Innocent Shio pamoja na wataalamu mbalimbali.