NA MWANDISHI WETU
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kupitia Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Miundombinu, Mhandisi Leopard Runji, imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ikiwemo ujenzi wa skimu ya Umwagiliaji Makwale, iliyopo Kyela mkoani Mbeya.
Katika ziara hiyo Mhandisi Runji ameeleza kuridhishwa na kazi inayoendelea na kumtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuongeza nguvu ili kukamilisha mradi kwa wakati.
Mhandisi Runji ameeleza kuwa mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 20.9 za kitanzania na utekelezaji wake umefikia asilimia 60.3, huku mkandarasi akiwa tayari amelipwa asilimia 50.8 ya malipo yake.
“Mradi huo unahusisha ujenzi wa banio, usafirishaji wa maji kupitia bomba lenye urefu wa kilomita 6.3, pamoja na mifereji mikuu na ya upili yenye zaidi ya kilomita 11. Aidha, kazi zilizokamilika ni pamoja na utandazaji na uungani wa Bomba kwa 5,454m (86.6%), Usakafiaji wa mfereji mkuu kwa kiwango cha zege kwa mita3150(63%) pamoja na Ujenzi wa vigawa maji kwa asilimia 60%, hivyo unaendana na thamani ya fedha iliyowekezwa.
“Mradi huu ni muhimu sana kwa wananchi wa Makwale. Bomba limejengwa kwa plastiki imara na linatarajiwa kunufaisha hekta 3,000 za mashamba. Ni jukumu letu sote kulinda miundombinu hii ili mradi huu ufikie malengo yaliyokusudiwa,” alisema Mhandisi Runji.
Mhandisi Runji amemtaja mkandarasi aongeze kikosi kazi ili kutumia vizuri muda uliosalia.
“Kazi ni nzuri, lakini kuna maeneo machache yanahitaji kuimarishwa zaidi, tuongeze nguvu kazi na kushirikiana kwa karibu ili kukamilisha mradi huu kwa wakati, tumechukua baadhi ya mahitaji mliyonayo tutayawasilisha kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ili kuendelea kutoa msukumo wa utekelezaji,” alisisitiza Runji.
Kwa upande wake, Mhandisi Macarius Mlayi kutoka kampuni ya Blue Mark, mkandarasi anayetekeleza mradi huo, alisema kazi imefikia zaidi ya asilimia 60 na tuihakikishie Serikali kupitia Tume na wananchi kuwa mradi utakamilika mwezi Desemba mwaka huu.
Amezitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni uwepo wa maji mengi katika eneo la bonde linalofanyiwa kazi, hali inayosababisha ucheleweshaji wa baadhi ya ujenzi hasa nyakati za mvua.
“Pamoja na changamoto hizo, tunaamini kwa kasi tuliyonayo na vifaa tulivyonavyo, mradi utakamilika kwa muda uliopangwa,” alisema Mlayi.
Baadhi ya wananchi wa eneo la Makwale akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Skimu ya Umwagiliaji Makwale,Bruno Benedicto Mwakalyobi
ameeleza matumaini waliyonayo kutokana na ujenzi wa mradi huo ukikamilika kuwa utawapa wakulima fursa ya kuzalisha mara mbili kwa mwaka bila kutegemea mvua.
“Tunaenda kupata neema ya kilimo cha Umwagiliaji cha uhakika, hivyo mavuno yetu yataongezeka na maisha ya wakulima kubadilika. Kilichobaki ni kuiomba Serikali yetu kuhakikisha wakulima tunapata pembejeo kwa wakati,” alisema Mwakarebi.
Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Makwale ukikamilika, unatarajiwa wakulima zaidi ya 20,000 hivyo kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kufungua fursa za kiuchumi kwa wakulima wa eneo hilo na mkoa wa Mbeya kwa ujumla.