

Mhe. Msando alisema kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015 kumewezesha taifa kupunguza gharama kubwa za matibabu nje ya nchi, huku Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiendelea kuwekeza kwenye vifaa tiba vya kisasa vinavyorahisisha huduma kwa kuendana na teknolojia za kisasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alisema taasisi hiyo imeendelea kujikita katika kutoa huduma za kibingwa ndani na nje ya nchi, na kwa sasa imekuwa hospitali ya rufaa ya kikanda barani Afrika. Amesema wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na hata nje ya bara hilo wanapatiwa huduma za moyo hapa nchini, jambo linaloonesha mchango wa taasisi hiyo katika kuokoa fedha na kuimarisha huduma za afya barani Afrika.
Katika hafla hiyo, Benki ya NMB ilitambuliwa na kukabidhiwa tuzo maalum kutokana na mchango wake mkubwa katika kusaidia juhudi za taasisi hiyo. Mwaka 2024, NMB na JKCI walisaini makubaliano ya ushirikiano wa Sh. bilioni 1 kwa kipindi cha miaka minne kusaidia gharama za matibabu ya watoto wanaopatiwa huduma katika taasisi hiyo — sawa na Sh. milioni 250 kwa mwaka.
Kwa kutambua jukumu lake katika maendeleo ya kijamii na kiafya, NMB Bank imeendelea kushirikiana na wadau muhimu kuboresha maisha ya Watanzania kupitia uwekezaji kwenye sekta ya afya.