Washirika wa kimataifa wametakiwa kutimiza ahadi zao ambazo wamekuwa wakizitoa katika majukwaa ya kimataifa kuhusu fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Philip Mpango wakati akihutubia Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika kuhusu Tabianchi jijini Addis Ababa, Ethiopia Septemba 08, 2025.
Akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mpango amesisitiza kuwa wakati Afrika ikichangia chini ya asilimia 4 ya hewa chafu duniani, bara la Afrika linaathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi kutokana na ukame, mafuriko, na kupanda kwa bahari na huku akiwaomba viongozi kukumbuka Azimio la Nairobi ambalo lilizaliwa katika Mkutano wa kwanza wa Kilele mwaka 2023.
Azimio la Nairobi liliweka msimamo wa pamoja wa Afrika kuhusu fedha za mabadiliko ya tabianchi, kukabiliana na hali hiyo, matumizi ya nishati mbadala na uanzishwaji mapinduzi ya kijani ya viwanda.
“Bila ya usaidizi wa haraka na wa hali ya juu, matarajio yetu ya ustahimilivu na maendeleo ya kijani yanabaki hatarini,” amesema Makamu wa Rais, akiyataka mataifa yaliyoendelea kuongeza kiasi cha mfuko wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuufanyia kazi Mfuko wa Hasara na Uharibifu, na kuhakikisha marekebisho yanapewa kipaumbele sambamba na COP30 nchini Brazil.
Makamu wa Rais, Dkt. Mpango ameitaja mipango mikubwa ya Tanzania inayoendana na mahitaji ya sasa ikiwa ni pamoja na Dira ya Taifa 2050, Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), na kupanua uwekezaji wa nchi katika nishati mbadala, nishati safi ya kupikia na uchumi wa bluu.
Kama Mwenyekiti wa sasa wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN)), Tanzania imeahidi kukuza sauti ya Afrika katika COP30 nchini Brazili, kuhakikisha vipaumbele vya Bara la Afrika vinapewa umuhimu.