Na Rahma Khamis, Maelezo.
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwa waangalifu katika kuandika Habari za Uchaguzi ili kuepusha uchochezi na uvunjifu wa Amani katika kipindi Chote Uchaguzi Mkuu unayotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji George Joseph Kazi katika Ukumbi wa Tume hiyo Maisara katika Mafunzo ya wadau wa habari wa Uchaguzi Mkuu.
Amesema kuwa lugha ya mwandishi inaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani au ni yenye kudumisha Amani hivyo ni vyema kuzingatia maadili, haki na wajibu katika kazi zao.
Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni matayarisho ya kuelekea Uchaguzi Mkuu ambapo waandishi wa habari wanatakiwa kutambua Sheria na kanuni katika kuandika habari za Uchaguzi.
Aidha amewashukuru wanahabari kwa kuwapatia wananchi taarifa za Tume ya Uchaguzi muda wote kuanzia uwandikishaji wa daftari la wapiga kura hadi kufikia sasa.
Akitoa taarifa kuhusu matayarisho ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2025 Mkurugenzi wa Tume hiyo Thabit Idarus Faina amesema wadau wa Uchaguzi wana haki na Wajibu wa kuhakikisha Uchaguzi unafanyika kwa salama na Amani.
Aidha ameeleza kuwa huo ni Uchaguzi wa saba tangu kuanza kufanyika mwaka 1992 kuanza kwa mifumo wa vyama vingi ambapo kila unapomaliza uchaguzi mmoja Tume inaandaa matayarisho ya Uchaguzi mwengine.
Akiwasilisha Wajibu na Maadili ya waandishi wa Habari wakati wa Uchaguzi Kaimu Mkurugenzi wa Habari Maelezo Asha Abdi Makame amesema kuwa muandishi ana wajibu kufuatilia na kuripoti Kampeni kwa usawa pamoja na kutoa fursa sawa kwa wagombea wa vyama vyote bila ya upendeleo.
Nao wadau wa Uchaguzi wameiomba Tume ya Uchaguzi na Tume ya Utangazaji Zanzibar kushirikiana na Jeshi la polisi ili kufanya kazi zao kwa ufanisi bila ya usumbufu wowote.