Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akishirikiana na wenzake wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) kumfanyia mtoto upasuaji wa kuziba tundu lililopo kwenye moyo na kufungua mshipa wa kupeleka damu kwenye mapafu ulioziba (Tof repair) wakati wa kambi maalumu ya siku 6 iliyoanza jana katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).
Madaktari bingwa wa usingizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Loth, Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia Michael Kangwa na mwenzao kutoka nchini Ethiopia Senait Kifle wakimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mtoto ambaye ana tundu kwenye moyo wakati wa kambi maalumu ya siku 6 ya upasuaji wa moyo iliyoanza jana katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).
Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia wakimkabidhi mtoto katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) mara baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuzibua mshipa wa kupeleka damu kwenye mapafu uliokuwa umeziba (Tof repair) na kuziba tundu lililopo kwenye moyo wakati wa kambi maalumu ya siku 6 iliyoanza jana katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).Picha na JKCI
……..
Na Mwandishi Maalum – Lusaka, Zambia
Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameanza rasmi kambi maalumu ya upasuaji wa moyo ya siku sita inayokwenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wataalamu wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).
Akizungumza kuhusu kambi hiyo leo jijini Lusaka, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa Watoto kutoka JKCI Godwin Sharau, alisema kupitia kambi hiyo watafanya upasuaji mgumu na wa kipekee kwa watoto waliokuwa hawana nafasi ya kupata huduma hizo nchini humo kabla ya kuanza kwa kambi hiyo ya matibabu.
“Kuna watoto tutakaowafanyia upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba (TOF repair), wengine waliozaliwa bila chumba cha moyo cha kulia kukua, na pia wale ambao valvu zao za moyo hazikujitengeneza vizuri. Pia tutawafanyia upasuaji watoto waliochelewa kupata matibabu na mapafu yao kuharibika, ili kuyasaidia yapone,” alisema Dkt. Sharau.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa watoto wa NHH Mudaniso Ziwa alisema kufanyika kwa kambi hiyo ni fursa kubwa ya kuongeza maarifa kwa madaktari wa Zambia na kuimarisha hadhi ya hospitali yao.
“Kupitia kambi hii, wataalamu wetu wanajifunza mbinu mpya ambazo hawajawahi kushuhudia. Tunaamini baada ya mafunzo haya tutaweza kujitegemea na kufanya upasuaji huu sisi wenyewe,” alisema Dkt. Ziwa.
Aidha, Dkt. Ziwa alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa ushirikiano baina ya JKCI na Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel, ili kila mwaka kuweze kufanyika kambi kama hizo zitakazoongeza ujuzi na kupunguza idadi ya watoto wanaosubiri upasuaji wa moyo nchini Zambia.
Dkt. Michael Kangwa, bingwa wa usingizi kwa watoto wa NHH, alisema kambi hiyo imemfundisha namna bora ya kuwatambua wagonjwa mapema na kufanya maamuzi ya haraka kabla hali haijawa mbaya.
“Nimejifunza mengi kwa kushirikiana na daktari bingwa wa usingizi kutoka JKCI ambaye naye alipata mafunzo yake kupitia SACH. Tunaposhirikiana tunakuwa na mipango inayofanana na kufanya huduma zetu kuwa bora zaidi”, alisema.
Naye Afisa Uuguzi wa chumba cha wagonjwa waliopo katika uangalizi maalumu (ICU) wa NHH Dorcas Mwape alisema kupitia kambi hiyo wauguzi wamepata ujuzi wa namna ya kuwahudumia wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo na atatumia maarifa hayo kuboresha huduma za kila siku kwa wagonjwa.
Kambi hiyo iliyoandaliwa na shirikia la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel imezidi kuimarisha ushirikiano kati ya wataalamu wa afya wa Zambia na Tanzania, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo wanapata huduma bora bila kulazimika kusafiri nje ya nchi.