MBUNGE wa Zamani wa Jimbo la Ilongero Lazaro Nyalandu ameonesha dhamira ya kweli ya kumtafutia kura mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake ya kupita Kijiji kwa Kijiji kumuombea kura.
Hatua hiyo kwa mujibu wa wadadisi mbalimbali wa masuala ya Kisiasa, anafaa kuwa mfano wa kuigwa kwani wapo baadhi ya waliokuwa wagombea wa nafasi ya Ubunge na Udiwani ambao kura hazikutosha au majina yao kukatwa wamesusianushiki wa uchaguzi huo na wengine wakidiriki hata kukihama Chama hicho.
Mbali na kumuombea kura Dk Samia Suluhu Hassan Nyalandu ambaye alishika nafasi ya pili katika mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi ya Ubunge pia anaitumia nafasi hiyo kwa kumnadi na kumuombea kura mgombea wa Ubunge wa Jimbo hilo Haidary Gulamali.
Nyalandu ambaye pia amewahi kushika nafasi ya Uwaziri wa Maliasili na Utalii, tangu kuzinduliwa rasmi kwa Kampeni za uchaguzi wa Chama hicho, amekuwa mstari wa mbele kwa kupita maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Singida na ambayo wagombea kupitia Chama hicho kupiga kampeni zao.
“Kimsingi Nyalandu ameonesha ukomavu ndani ya Chama, hajaonesha kama alikuwa anagombea ili Kupitishwa, kwani licha ya jina lake kutopita yupo mstari wa mbele kuwaombea kura wagombea wengine kupitia CCM, huu ni mfano wa kuigwa wa ukomavu Kisiasa” alisema mmoja wa wananchi aitwaye Athumani Sinda
Alisema mbali na Kampeni mwanasiasa huyo amekuwa mstari wa mbele kwa kuhamasisha uzalendo ambapo kupitia Kampeni ya ‘Vijana na Tanzania’ wamepita mikoa mbalimbali kuhamasisha uzalendo na upendo kwa Rais Samia.