Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani wametakiwa kulitunza na kulithamini zao la kahawa kwa kuligeuza kuwa fursa ya kiuchumi itakayowainua wao binafsi na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Septemba 10, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Kahawa la Msimu wa Sita, lililofanyika mkoani humo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, RC Babu amesema kuwa Mkoa wa Kilimanjaro unatambulika kitaifa na kimataifa kupitia zao la kahawa, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu kulilinda na kulitumia kikamilifu.
“Kahawa ni utambulisho wa mkoa wetu. Tusipoitunza na kuitumia kama fursa ya maendeleo, tutapoteza hazina kubwa sana,” amesema Babu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Primus Kimario, amesema kuwa malengo ya tamasha hilo ni kuwawezesha wananchi kutumia fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa zao hilo, pamoja na kutoa elimu kuhusu faida za kiafya na kiuchumi zitokanazo na kahawa.
“Katika msimu huu wa sita, tutalenga zaidi kutoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia mpya katika kilimo cha kahawa na namna ya kuifikia masoko ya kimataifa,” amesema Kimario.
Naye mkulima wa kahawa kutoka mkoani humo, Julius Mollel, amepongeza tamasha hilo na kuomba wataalamu wa kilimo waendelee kutoa elimu kwa wakulima vijijini ili kuongeza uelewa kuhusu faida za kahawa katika maendeleo ya mtu binafsi na taifa.
“Wakulima wengi bado hawajui thamani halisi ya zao hili. Tunahitaji mafunzo ya mara kwa mara ili tuweze kulima kibiashara na kwa tija,” amesema Mollel.
Tamasha hilo limekusanya wadau mbalimbali kutoka sekta ya kahawa, wakiwemo wakulima, wanunuzi, wasindikaji na taasisi za utafiti wa kilimo, likiwa na kaulimbiu ya “Kahawa ni Mali, Tuitunze na Tuitumie kwa Maendeleo.