

Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, ametuma salamu nzito kwa mashabiki wa klabu hiyo akisisitiza kuwa msimu mpya wa 2025/26 ni wa ushindani wa kweli na lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanabeba mataji makubwa.
Akizungumza katika tamasha la Simba Day 2025 lililofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Davids alisema:
“Msimu uliopita ulikuwa ni msimu wa kujenga msingi, msimu huu ni kwa ajili ya kubeba mataji, msimu wa kushindania mataji.”

Kauli hiyo imepokelewa kwa shangwe na mashabiki waliomiminika kwa wingi kushuhudia tukio hilo kubwa la kila mwaka. Simba, ambao wanashiriki tena Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Mabingwa Afrika, wamefanya usajili wa wachezaji wapya wenye viwango vya kimataifa na kuimarisha benchi la ufundi kwa lengo la kurejesha heshima ya klabu hiyo.
Tamasha la Simba Day mwaka huu limeendelea kuonesha ukubwa na hadhi ya klabu hiyo, si tu kama timu ya mpira wa miguu, bali pia kama taasisi ya kijamii inayojikusanyia mamilioni ya mashabiki.
Kwa kauli ya Davids, mashabiki wa Simba sasa wana kila sababu ya kutazama msimu mpya kwa matumaini makubwa, wakiamini kikosi chao kimeiva kwa mapambano ya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.









