NA WILLIUM PAUL, MWANGA
WANANCHI zaidi ya 1650 wa vitongoji vya Stesheni, Mforo na Kichwang’ombe wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wameondokana na hadha ya kutumia maji yasiyo safi na salama baada ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Same – Mwanga (SAMWASA) kufikisha huduma ya maji safi na salama.
Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi wa mamlaka hiyi, Mhandisi Rashidi Mwinjuma kwa Mkuu wa wilaya ya Mwanga Rukia Zuberi alipofika kujionea utekelezaji wa mradi huo ambapo alisema kuwa, kabla ya ujenzi wa mradi huo wakazi wa vitongoji hivyo walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 6 kufuata maji katika kituo cha maji cha zahanati ya Kisangiro.
Mhandisi Mwinjuma alisema kuwa, wakati mwingine walikua wanalazimika kutumia maji ya mto jirani ambayo hutiririka wakati wa mvua ambapo yalikuwa yakitumiwa pia na mifugo.
“Kufuatia changamoto hii SAMWASA ilifanya usanifu wa mradi wa kuendeleza mtandao wa mabomba katika vitongoji hivi na kwa ushirikiano wa wadau tumefanikiwa kutekeleza ujenzi wa mradi ambapo ambapo tumeunganisha maji katika kaya 30 pamoja na kujenga vilula vitano” Alisema Mhandisi Mwinjuma.
Alisema kuwa, mradi huo umegharimu shilingi milioni 37.5 ambapo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mwanga walinunua mabomba na vifaa vya maunganisho ya maji vya shilingi milioni 25.7, SAMWASA walinunua Dira za maji, usimamizi na ufundi unaogharimu shilingi milioni 6 na wananchi walijitolea kuchimba na kufikia mitaro kwa gharama ya milioni 5.7.
Aliongeza kuwa, kupatikana kwa mradi huo utasaidia upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama na ya uhakika pamoja na kukuza fursa ya uwekezaji na kukuza uchumi katika vitongoji hivyo wilaya na Taifa.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi, kutunza miundombinu ya maji, pamoja na kulipa ankara za maji kwa wakati huku pia akiwataka kujitokeza kuomba huduma ya maunganisho ya maji katika kaya binafsi na taasisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mwanga, Rukia Zuberi alisema kuwa, lengo la serikali ya awamu ya sita ni kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo tatizo la maji na kuwataka kuhakikisha wanaulinda mradi huo ili uweze kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Rukia alisema kuwa, ni jukumu la kila mwananchi kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha kuwa huduma inaendelea kuwepo ikiwemo kulinda miundombinu ya maji pamoja na kulipa ankara za maji.