Mkuu wa Kitengo cha Utawala wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joachim Asenga akitoa mafunzo ya wajibu wa mtumishi wa umma kwa wafanyakazi 149 waliokuwa chini ya hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS – Dar Group) kabla haijakabidhiwa kwa JKCI Novemba 2022 ambao wote wamepata ajira serikalini Agosti mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda akizungumza na wafanyakazi 149 waliokuwa chini ya hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS – Dar Group) kabla haijakabidhiwa kwa JKCI Novemba 2022 ambao wote wamepata ajira serikalini Agosti mwaka huu.
Mchunguzi Mkuu Kiongozi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ilala Nerry Mwakyusa akitoa elimu ya madhara ya rushwa mahali pa kazi kwa wafanyakazi 149 waliokuwa chini ya hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS – Dar Group) kabla haijakabidhiwa kwa JKCI Novemba 2022 ambao wote wamepata ajira serikalini Agosti mwaka huu.
Baadhi ya wafanyakazi waliokuwa chini ya hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS – Dar Group) kabla haijakabidhiwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Novemba 2022 ambao wote wamepata ajira serikalini Agosti mwaka huu wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinatolewa katika mafunzo elekezi ya siku tatu kwa watumishi waliopata ajira ya kudumu serikalini. (Picha na JKCI)
………………
Na mwandishi Maalumu, Dar es Salaam.
Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imewaajiri wafanyakazi 149 waliokuwa wafanyazi wa Hospitali ya Dar Group kabla haijakabidhiwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tarehe 15 Novemba 2022.
Kabla ya kukabidhiwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wafanyakazi hao walikuwa chini ya hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS – Dar Group).
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Idd Lemah wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku tatu kwa watumishi waliopata ajira ya kudumu serikalini.
Lemah alisema serikali iliwapatia Hospitali ya Dar Group iliyopo wilayani Temeke kuwa sehemu ya JKCI. Kuwepo kwa hospitali hiyo kumetatua changamoto ya nafasi ambayo walikuwa wanakabiliana nayo kwa muda mrefu na kusaidia kuboresha huduma za matibabu wanazozitoa kwa wananchi.
“Serikali ilitukabidhi hospitali hii ikiwa na majengo, mali, watumishi na madeni. Baada ya kufanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi tumeweza kuwaajiri wafanyakazi wote na leo tunatoa mafunzo haya ili kuhakikisha wanazingatia sheria, taratibu, weledi na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kuepekana na vitendo vya rushwa”.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wafanyakazi hawa na kuwapatia ajira ninaamini walivyokuwa wanatoa huduma bora wakati wako katika sekta binafsi wataendelea kutoa huduma hiyohiyo serikalini”, alisema Lemah.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Utawala wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Joachim Asenga alisema mafunzo hayo ya siku tatu kwa wafanyakazi hao yamelenga kuwajengea mbinu bora za uwajibikaji katika kazi zao za kila siku.
“Kutolewa kwa mafunzo haya ni takwa la kisheria kwa watumishi waliopata ajira serikalini, watafundishwa mada mbalimbali zikiwemo za madhara ya rushwa mahali pa kazi, haki na wajibu wa mtumishi katika utumishi wa umma, na Usalama wa Taifa”, alisema Asenga.
Akizungumza wakati akitoa mada ya madhara ya rushwa mahali pa kazi Mchunguzi Mkuu kiongozi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ilala Nerry Mwakyusa alisema kutolewa kwa mafunzo kuhusiana na rushwa kutawasaidia waajiriwa wapya kutambua madhara ya rushwa mahali pa kazi na jinsi ya kuiepuka.
“Dhana ya kwamba wale wanaotoa rushwa ya fedha ndiyo wanaoweza kupata huduma katika sekta ya afya ni kinyume cha sheria na inaweza kusababisha vifo kwa watu watakaoshindwa kutoa fedha kwani watachelewa kupata huduma ambayo ingeokoa maisha yao”, alisema Nerry.
Nao wafanyakazi waliohudhuria mafunzo hayo walishukuru kwa nafasi waliyoipata ya kupata ajira Serikalini na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa na wananchi wanaowahudumia.
“Tunashukuru tangu tumekabidhiwa kwa JKCI maslahi yetu yameboreshwa na tumeajiriwa serikalini, tutaendelea kutoa huduma za kizalendo kuhakikisha matokeo makubwa yanaonekana na kuifanya hospitali hii kuwa ya mfano wa kuigwa” alishukuru Daktari Bingwa wa magonjwa yatakanayo na kazi Elias Birago.
“Kabla sijaajiriwa serikalini ilinilazimu kila baada ya muda fulani kujaza fomu za mkataba wa ajira kitu ambacho kilikuwa kinaniletea mawazo kwani kuna wakati unafikiria kama unaweza kupata mkataba au la. Ninashukuru kwa ajra niliyoipata na ninaahidi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora zaidi”, alisema Afisa Tehama Mary Vyabula.