Na Mwandishi wetu, Babati
MKUU wa Mkoa wa Manyara (RC), Queen Cuthbert Sendiga amewatakia kila la heri wanafunzi wote wa darasa la saba wa eneo hilo watakaofanya mtihani wao wa kuhitimu darasa la saba kwa siku mbili.
RC Sendiga amewatumia salama za kuwatakia heri wanafunzi hao wa Mkoa wa Manyara watakaofanya mtihani kwa siku mbili za jumatano Septemba 10 mwaka 2025 na alhamisi Septemba 11 mwaka 2025.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara (RAS), Maryam Muhaji amesema wanafunzi 38,859 katika shule za msingi 700 wanatarajia kufanya mtihani kwenye mkoa huo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro (DED) Gracian Max Makota amesema wanafunzi 5,617 wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba.
Makota amefafanua kwamba wanafunzi hao watafanya mtihani kwenye shule za serikali 85 zenye wanafunzi 5,267 na binafsi shule 11 zina wanafunzi 350.
Mkurugenzi wa mji wa Mbulu, Rehema Bwasi amesema wanafunzi 3,217 watafanya mtihani kwenye shule 58 zilizosajiliwa.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ Teresia Ifafay amesema wanafunzi 7,869 watafanya mtihani kwenye shule 130 za serikali na nane za binafsi.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu vijijini Abubakari Kuuli amesema wanafunzi 5066 wavulana 2,207 na wasichana 2,859 wanatatajia kufanya mtihani kwenye shule 101.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mirerani Mwanaisha Adam amesema anamshukuru Mungu kwa wanafunzi wake 137 ambao wamefanya mitihani yao mitatu kwa siku ya kwanza.
Mwalimu Mwanaisha ameeleza kwamba, awali wanafunzi 139 waliandikishwa kwa ajili ya kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba ila wawili wakawa watoro.
“Tunamshukuru Mungu wanafunzi wetu wamefanya mitihani salama ila mmoja alipata changamoto ya tumbo akapewa dawa kisha akaendelea vyema,” ameeleza.
Mmoja kati ya wanafunzi wa shule ya msingi Mirerani, Losioki Mola amesema amefanya mitihani mitatu ya kiswahili, hisabati na maarifa ya jamii na anatarajia atafaulu vyema.
Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo Rehema Mecksela ameeleza kwamba matarajio yake ni kufaulu na kwenda shule ya sekondari mwakani 2026.