Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) kutoka Wizara ya Nishati Anitha R. Ishengoma, amesema Wizara imejipanga kwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha sekta ya nishati inaboresha upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu kwa Watanzania.
Akizungumza katika Kongamano la Nne la Kitaifa la Ufuatiliaji na Tathmini jijini Mwanza, Ishengoma amesema hatua ya kwanza ilikuwa ni kuelewa wigo wa tathmini na majukumu ya sekta, ili kufahamu walipo na wanapotaka kufika, amefafanua kuwa Wizara imejikita kwenye maeneo makuu matatu ya nishati ambayo ni mafuta, gesi na umeme, ambayo yote yanachangia katika jukumu kubwa la kusambaza nishati bora, nafuu na ya uhakika.
“Baada ya kujua majukumu yetu makubwa na kufahamu kuwa nishati ni injini ya uchumi, tulilazimika kuangalia sekta zenye kipaumbele zilizotajwa kwenye mpango mkakati wa Wizara na mipango ya muda mrefu ya serikali, Hapo ndipo tukaona namna taasisi zilizo chini ya Wizara zinavyoweza kutekeleza majukumu yao kwa mpangilio unaoendana na malengo ya kitaifa,” alisema.
Amesema sekta ya nishati inahusisha taasisi kubwa sita ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la kuagiza mafuta nchini, pamoja na mamlaka mbili za udhibiti, huku pia kukiwa na kampuni tanzu tano (subsidiaries).
Ishengoma ameongeza kuwa kila robo mwaka Wizara hufanya vikao vya menejimenti vinavyoongozwa na Waziri mwenyewe, ambapo hujadili changamoto za kila idara, kufahamu maeneo yenye mapungufu na kuibua mikakati ya kuboresha utendaji.
“Vikao hivi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha tunaboresha maeneo yenye changamoto na kuimarisha huduma kwa wananchi.”
Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa serikali, taasisi za umma na sekta binafsi, likilenga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kwa maendeleo endelevu nchini.