Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MANISPAA ya Mji Kibaha, mkoani Pwani Pwani, imejipanga kufungua shule mpya tatu za sekondari na kununua madawati 2,000 ikiwa ni miongoni mwa maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2026.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dk. Rogers Shemwelekwa, alieleza mikakati hiyo septemba 13,2025 wakati wa Mahafali ya 20 ya elimu ya msingi ya shule zilizo chini ya Taasisi ya Njuweni Institute, ikiwemo Kibaha Independent School (KIPS) Main, Annex na Msangani KIPS.
Dk. Shemwelekwa alieleza, miundombinu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa imeongezeka huku Manispaa ikijiandaa kufungua shule mpya za sekondari Muungano, Tangini na Msangani II, zitakazopokea wanafunzi kuanzia Januari 2026.
Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanajiandaa kuwapeleka watoto wao shule bila kuwaacha majumbani, kwa kuwa elimu ya sekondari ni bure na ni haki ya kila mtoto.
Kuhusu changamoto ya barabara korofi, Shemwelekwa alieleza, Manispaa hiyo imetenga kiasi cha sh. milioni 520 kwa ajili ya kufungua barabara za ndani ambazo hazipitiki kirahisi, ikiwemo barabara za Mtaa wa Lumumba na Mkombozi zilizopo Kata ya Pangani.
Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Kibaha, Adinani Livamba, alisema kuwa kwa mwaka huu jumla ya wanafunzi 6,537, wakiwemo 1,132 kutoka shule binafsi, wamehitimu elimu ya msingi.
Awali, Mkurugenzi wa Makampuni ya Njuweni, Alhaj Yusufu Mfinanga, aliahidi kutoa ufadhili kwa wanafunzi 12 watakaofaulu kwa daraja A ili kujiunga na shule za sekondari za taasisi hiyo zikiwemo Vuchama, Ugweno Islamic zilizopo Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya KIPS Annex, Ramadhan Kitambi, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita shule hizo zimeendelea kufanya vizuri kitaaluma katika ngazi ya Manispaa, Mkoa na Taifa, kwa kupata ufaulu wa daraja.