Wazalishaji wa miche ya kahawa katika kijiji cha Ndilimalitembo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wakiondoa majani na uchafu ili kubakisha miche bora ya kahawa kabla ya kusambazwa kwa wakulima wa zao hilo.
Afisa Ushirika wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Given Malik wa pili kulia,akizungumza na baadhi ya wazalishaji miche bora ya Kahawa wa kijiji cha Ndilimalitembo jana,baada ya kukagua kitalu cha miche bora ya kahawa inayozalishwa na Chama cha msingi cha Ushirika Mkombozi Amcos.
…….
Na Mwandishi maalum, Songea
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,imeanza rasmi kuwekeza kwenye kilimo cha zao la kahawa kwa kuwapatia wakulima miche bora ya kisasa ili kuongeza uzalishaji, kuwainua wakulima kiuchumi na Manispaa iweze kuongeza mapato yake.
Afisa Ushirika wa Manispaa ya Songea Given Malik amesema,kupitia idara ya Ushirika wanashirikiana na wadau wengine wakiwemo Taasisi ya utafiri wa kahawa Tanzania(TACRI)na Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB) kutatua changamoto walizonazo wakulima wa kahawa kwa kutafuta ufumbuzi wa upatikanaji wa mbegu bora,madawa na masoko.
“Sisi kama Serikali kupitia Manispaa yetu ya Songea,tumeanza mkakati wa kufufua zao la kahawa kwa kuwatembelea wakulima wote waliojiunga kwenye vyama vya msingi vya ushirika ili kuwawawezesha kuongeza uzalishaji,kupata uhakika wa mbegu,madawa na kuwatafutia masoko ya uhakika”alisema Malik.
Amesema,mkakati wa kufufua zao la kahawa umepokelewa vizuri na wakulima katika Manispaa ya Songea kwa sababu wana matumaini makubwa ya kufufuka kwa zao hilo ambalo kwa muda mrefu halikuwa na usimamizi nzuri hivyo kushindwa kuleta tija kwa wakulima na Serikali.
Kwa mujibu wa Malik,Programu ya kuwahamasisha wakulima kufufua mashamba ili kuongeza uzalishaji utasaidia hata kushawishi wakulima wengi kurudi na kuwekeza tena kwenye zao hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Songea itaendelea kuwatambua na kuwaweka pamoja wakulima wote ili kuhakikisha wanaingia na kujiunga kwenye ushirika ambao ili iwe rahisi kwao kupewa huduma mbalimbali za ugani na elimu.
“Jukumu lingine tunalolifanya kama Serikali ni kuwahamasisha wananchi ambao hawana elimu ya ushiriki wafahamu ushirika ni nini na faida zake na baadaye tunafanya utaratibu wa kuanzisha vyama na kuvisimamia ili waweze kupata mikopo ya pembejeo,fedha kwa ajili ya shughuli zao za kilimo na elimu ya ushirika kwa ujumla”alisema Malik.
Amesema,dhana ya ushirika ina maana kubwa na nzuri na ikitiliwa mkazo kama inavyofanya Serikali ya awamu ya sita wakulima watafika mbali kimaendeleo na kiuchumi kwa kuwa changamoto nyingi zilizokuwa hapo awali zimeanza kutatuliwa na Serikali imeweka nguvu kubwa katika sekta ya ushirika.
Malik amesema,zao hilo lina mchango mkubwa kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja,Halmashauri,Taifa na kwa maendeleo ya jamii lakini katika Manispaa ya Songea limeonekana kuzorota na kutokuwa na mchango wowote kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
Amesema,ili kuongeza uzalishaji wenye tija Manispaa ya Songea kupitia idara ya ushirika imejipanga kuimarisha upatikanaji wa miche bora kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima na amewapongeza wakulima wa kata ya Ndilimalitembo kwa kuanzisha kilimo cha kahawa.
Moses Komba mwanakikundi kinachojihusisha kuzalisha miche ya kahawa katika Kijiji cha Ndilimalitembo amesema,changamoto kubwa waliyonayo katika uzalishaji wa zao hilo ni upatikanaji wa mbegu hali inayopelekea kuzalisha miche kidogo huku mahitaji ya wakulima ni makubwa.
Komba ameiomba Serikali kupitia Taasisi ya utafiti wa Kahawa(TACRI) na Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB),kutoa ruzuku kama ilivyo kwenye vikundi vingine ili waweze kuzalisha miche mingi ambayo watasambaza kwa wakulima wengi zaidi wenye nia ya kulima zao hilo.
“tunaishukuru sana Serikali kutupatia pembejeo za ruzuku hasa kwenye zao la mahindi ambazo zimetusaidia sisi wakulima kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji,lakini tunaomba mpango huo wa ruzuku ufanyike hata kwetu sisi wazalishaji wa miche ya kahawa”alisema Komba.
Editha Hyera,mjumbe wa bodi ya Chama cha msingi cha Ushirika Mkombozi Amcos amesema,ni kukosa mashine ya kupuliza madawa na mikasi kwani kwa sasa wana mashine mbili tu ambazo zinatumiwa na wakulima wote wanaolima kahawa katika kata ya Ndilimalitembo.
Amesema,uwezo wa kikundi chao kuzalisha miche bora ya kahawa bado ni mdogo,hivyo ameiomba Serikali kuwaongezea nguvu ya fedha na vifaa ili waweze kuzalisha miche mingi itakayowafikia wakulima wengi.