NA DENIS MLOWE, IRINGA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amezindua mbio za ubungev Iringa mjini kwa kumnadi Mgombea Ubunge Jimbo la Iringa Mjini Fadhili Ngajilo mbele ya mamia ya wananchi katika mkutano uliofanyika kiwanja cha Mwembetogwa.
Katika mkutano huo wa uzinduzi iliyohudhuriwa na umati wa wanachama na wakazi wa Iringa, Wasira alimtambulisha rasmi mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, pamoja na madiwani wa CCM watakaowania kata mbalimbali za jimbo hilo.
Akihutubia wakazi wa Iringa, Wasira alisema kuwa wananchi wa Iringa Mjini tayari wamewahi kuonja uongozi wa vyama vya upinzani kama NCCR Mageuzi na Chadema, na kwamba CCM haiwalaumu kwa maamuzi yao ya awali kwa kuwa mamlaka hutoka kwa wananchi, lakini safari hii wana kila sababu ya kurejesha imani yao kwa CCM kwa nafasi ya Rais, Mbunge na Madiwani.
Alisema CCM ni chama chenye ajenda pana zinazogusa maisha ya kila Mtanzania, zikiwemo ajenda za umoja, amani, maendeleo na utekelezaji wa ahadi zinazopimika na kuonekana mbele ya wananchi.
Wasira alisema kuwa katika mkoa wa Iringa maendeleo yameonekana kwa vitendo ambapo chini ya serikali ya awamu ya sita ujenzi wa shule nne mpya za msingi na madarasa 114, sekondari nne mpya, madarasa 134 ya sekondari, pamoja na ujenzi wa zahanati tatu na vituo vya afya vitatu vilijengwa.
Aliongeza kuwa CCM imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya, barabara, nishati, pamoja na mapambano dhidi ya vifo vya kina mama wajawazito, na kwamba yote hayo ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama.
Alisisitiza kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 imejielekeza zaidi katika kutatua changamoto halisi za wananchi na iwapo wananchi wa Iringa Mjini wataichagua CCM, Wasira aliahidi kuwa kutajengwa shule mpya 22, vituo vya afya saba, zahanati 12, pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko (Bypass)na kwa upande wa uchumi, kiwanda cha kukoboa mahindi kilichosimama kitafufuliwa, na kilimo cha umwagiliaji kitaimarishwa.
Makamu Mwenyekiti huyo alihitimisha kwa kuwaomba wananchi kumpigia kura Rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge Fadhili Ngajilo na madiwani wote wa CCM huku akimkabidhi Ngajilo Ilani ya CCM pamoja na Ilani ya Jimbo la Iringa Mjini ili aweze kuwaongoza kwa mwelekeo sahihi.
Kwa upande wake, Fadhili Ngajilo, alipata nafasi ya kuhutubia wananchi na kukishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kumuamini na kumteua kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini akisema amejipanga kuwa sauti ya wananchi wa Iringa, na kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanyika mjini humo, wana kila sababu ya kuwa Jiji akimuomba Makamu kulifikisha Kwa mwenyekiti wa Chama Cha mapinduzi Taifa Dr.Samia suluhu Hassan.