Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ndugu Abeida Rashid Abdallah akizungumza katika kongamano la Utulivu wa Maisha ya ndoa lenye mada: Siri ya Ndoa yenye Sakina, Kongamano hilo limefanyika Septemba 13, 2023, katika hoteli ya Serena Dar es salaam na limeandaliwa na Jumuiya ya Khairun Nisaa Foundation
………………
Katika hotuba yake amesema ndoa yenye sakina/utulivu, inajenga msingi imara ndani ya familia na jamii, hivyo jukumu la kuhamasisha ndoa yenye sakini ni wajib wa kila mtu, familia, jamii na viongozi wa kitaifa kwa maendeleo ya taifa.
“Kila mmoja anawajibu wa kuhamasisha ndoa yenye Sakina katika kuhakikisha hatua madhubuti za kuimarisha maadili mema yanazingatiwa, sunnah na akhlaq njema” Amesema Katibu Mkuu huyo.
Ndugu Abeida amefahamisha siri zinazosaidia kuimarisha ndoa yenye baraka na thabiti, ikiwemo: Kumcha Allah na kuzingatia mipaka yake, upendo na huruma baina ya wanandoa na mawasiliano na uvumilivu katika changamoto. Pia amesema kuheshimiana na kushirikiana katika majukumu ya familia inaleta sakina/ utulivu katika ndoa.
Aidha amesema Wizara yake inafanya juhudi mbali mbali za kuelimisha jamii kuhusu malezi ya Watoto yanahitaji mashirikiano ya baba na mama katika malezi kwani yanaleta upendo ndani ya familia.
Amefahamisha kwa Wizara pekee hatoweza kufanikisha ndoa zisivunjeke lakini kwa mashirikiano kati Serikali na taasisi binafsi, hata mtu mmoja mmoja anapashwa kushiriki katika kuhamasisha masuala ya malezi bora ya familia.
Mwisho, ametoa pongezi za dhati kwa Khairun Nisaa Foundation kwa kuandaa jukwaa hili la kipekee. Ni furaha kuona wanawake na jamii kwa ujumla wakijitahidi kuboresha maisha yao kwa kuelimika na kuhamasika kuhusu masuala ya ndoa na familia.
Pia ndugu Abeida alimuomba Mwenyezi Mungu awaongoze wa umini katika kufuata wingo wa maisha ya ndoa na familia kama alivyokuwa bibi Aisha (R. A) Mke wa Mtume Muhammad (S.A. W).
Alimalizia kwa kusema Familia bora, Taifa Imara ni nguzo ya Maisha.