Na Meleka Kulwa -Dodoma
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imetoa wito kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma kuandika habari zenye Usawa kwa wagombea mbalimbali wanaoshiriki Katika Uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Aidha tume hiyo imewaasa waandishi kuacha kutoa maoni yoyote ama. Kuchapisha taarifa zozote ambazo zinayoweza kuleta chuki na uvunjifu wa amani, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu
Wito huo umetolewa leo Septemba 17,2025 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati wa mafunzo kwa Waandishi wa Habari kuhusu uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika mchakato wa uchaguzi mkuu 2025.
”Katika kipindi hiki cha uchaguzi, Waandishi wa Habari wanawajibu wa kuripoti matukio yote ya uchaguzi kwa usahihi bila upendeleo wowote kwa Chama, Mgombea au msimamo wowote wa Kisiasa na kuweka uwiano sawia wa taarifa kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi” amesema
Aidha, amewataka waandishi wa habari, kutumia mbinu madhubuti kwenye majukwaa kidigitali na vyombo vingine vya Habari ili kuepusha upotoshaji wa taarifa binafsi au kusema uongo juu ya Mgombea.
Aidha, amesema kuwa waandishi wa Habari wanawajibu wa kuepuka kutumia lugha ya matusi , kashifa kejeli na udhalilishaji pamoja na vitisho katika kuripoti matukio ya uchaguzi
Pia, amebainisha kuwa waandishi wa Habari, wanapaswa kujiepusha na rushwa na maudhui yenye kuegemea upande wa Chama au Mtu Fulani
Aidha, Jaji mstaafu, Mathew Mwaimu, ametoa rai kwa Waandishi wa Habari, kuepuka kuchapisha au kutangaza habari zenye nia ya kuchochea vurugu, ubaguzi au chuki za Kisiasa kikabila, kidini au kijinsia
Aidha, amewataka ifikapo siku ya kupiga kura, wajiepushe na kupiga kampeni , ikiwemo kuvaa mavazi yenye alama ya Chama au mgombea yoyote.
Pia, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu, ametoa wito kwa Waandishi wa Habari, kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya Kijamii, na kusema kuwa vyombo vya Habari vijikite katika kuimarisha amani, utulivu na demokrasia nchini.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (DPC) , Blaya Moses, amewataka waandishi wa Habari kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni na miongozo ya Uandishi wa Habari.