Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte akizungumza leo, Septemba 17, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua kikao cha wateja na wadau wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD, Victor Sungusia akitoa salama wakati akimkaribisha mgeni rasmi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte katika ufunguzi kikao cha wateja na wadau wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte, ameipongeza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake, huku akitoa wito kwa watendaji wa Manispaa kuhakikisha wanadhibiti na kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwezesha ulipaji wa madeni kwa wakati.
Akizungumza leo, Septemba 17, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua kikao cha wateja na wadau wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Mhinte amesema kuwa usimamizi mzuri wa mapato yatokanayo na huduma za afya ni muhimu katika kuhakikisha vituo vinaweza kununua bidhaa muhimu na kusimamia mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.
“Washiriki wa kikao hiki mna wajibu mkubwa wa kuhakikisha vituo vyenu vinakusanya mapato kikamilifu ili kuwa na uwezo wa kununua dawa na vifaa tiba kwa wakati,” amesema Mhinte.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongeza bajeti ya ununuzi wa bidhaa za afya ili kuboresha huduma kwa wananchi.
“Kikao hiki kina umuhimu mkubwa kwa kuwa kinaboresha uhusiano kati ya MSD na vituo vya kutolea huduma za afya, si tu kwa Mkoa wa Dar es Salaam, bali pia kwa nchi nzima,” ameongeza.
Mhinte amesema kikao hicho kinalenga kutoa uelewa zaidi kuhusu mifumo ya MSD, kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kushirikiana ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.
“Natarajia kikao hiki kitazaa maazimio ambayo utekelezaji wake utaimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na huduma bora katika vituo vyetu,” amesema Mhinte.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD, Victor Sungusia, amesema kuwa serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi bilioni 200 hadi bilioni 300 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za afya nchini.
“Tunaendelea kuboresha utendaji kazi wetu, kuhakikisha huduma inapatikana kwa wakati. Naomba washiriki wa kikao hiki mtoe mrejesho ili tuweze kuboresha zaidi,” amesema Sungusia.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Betia Kaema, amesema kuwa MSD inajenga mfumo madhubuti wa ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya kwa kutumia mbinu na ushauri wa kitaalamu.
“Tumefikia hatua ya kuingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji wa bidhaa za afya ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wakati,” amesema Kaema.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka kutoka asilimia 54 katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 74, na wanatarajia kufikia asilimia 90 katika mwaka wa fedha 2025/26.
Washiriki wa kikao hicho, akiwemo Mfamasia wa Manispaa ya Kinondoni Oswin Sanga na Mfamasia wa Manispaa ya Kigamboni Magreth Lali, wameishukuru Serikali kupitia MSD kwa maboresho makubwa yaliyochangia upatikanaji wa dawa, huku wakipendekeza kuimarishwa kwa baadhi ya mifumo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.