Na Jane Edward, Arusha
Wakulima wa zao la ngano wilayani Monduli, mkoa wa Arusha, wameiomba serikali iwasaidie kuwatafutia soko la jumla ili waweze kunufaika na jitihada la zao hilo.
Wakizungumza wakati wa sherehe za siku ya wakulima wa ngano zilizofanyika katika Kijiji cha Lendikinya, wakulima hao walisema licha ya jitihada kubwa wanazoweka shambani, bado changamoto ya soko imekuwa kikwazo kikuu kwao.
Mkulima wa zao hilo Metui Mollel na Rahama Laiza walisema wanajitahidi kulima kwa bidii lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa soko la uhakika na kwamba wanaomba serikali iwaunganishe na wanunuzi wakubwa ili waweze kunufaika na kilimo hicho.
“Ngano ni zao lenye manufaa makubwa, lakini wakulima wengi wameshindwa kuendelea kwa sababu ya masoko na akasisitiza kuwa iwapo serikali itawasaidia, wanaamini kilimo hicho kitaimarisha maisha yao”Walisema
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TARI Selian, Caresma Chuwa pamoja na Mtafiti Mtaalamu wa zao hilo Ismail Ngolinga,alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wakulima kwa karibu ili kuhakikisha teknolojia za kilimo cha kisasa zinafika vijijini na kuongeza kuwa ushirikiano huo ndio utakaowezesha kilimo cha ngano kuwa cha kibiashara.
Ameongeza kuwa Katika mafunzo hayo ya mashamba darasa, watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Selian walitoa elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora na mbinu sahihi za kuongeza uzalishaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Afisa Tarafa ya Kisongo, Tatu Furahisha, alisema serikali inatambua umuhimu wa siku ya wakulima wa ngano na itaendelea kushirikiana nao.