Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Hassani Mwamweta amefanya mazungumzo na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsch Welle (DW), Bw. Daniel Gakuga yaliyofanyika ofisi ya Ubalozi Septemba 18, 2025.
Bw. Gakuga aliyeambatana na Naibu wake, Bi. Grace Kabogo walifika ubalozini kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika nyadhifa hizo hivi karibuni.
Katika mazungumzo yao, Bw. Gakuga alitumia fursa hiyo kueleza mipango, majukumu na kazi mbalimbali zinazofanywa na DW.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Mwamweta alimpongeza kwa kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo na kumuahidi ushirikiano.
Wawili hao pia walijadili umuhimu wa vyombo vya habari katika kuhabarisha na kuelemisha kwa kuzingatia mazingira, mila, desturi na tamaduni za jamii husika.
DW Kiswahili ni kituo cha utangazaji cha Serikali ya Ujerumani kinachotoa habari za kila siku katika redio, runinga na mitandao ya kijamii kwa lugha ya Kiswahili zikilenga wasikilizaji na watazamaji katika nchi za Afrika Mashariki na Ukanda wa Maziwa Makuu. DW hushirikiana na vituo vya redio vya washirika katika nchi mbalimbali.
Inakadiriwa kuwa takribani asilimia 80 ya wasikilizaji wa DW idhaa ya kiswahili wapo nchini Tanzania.