Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Ashura Katunzi akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Septemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam.
……………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetenga jumla ya shilingi 36,802,360,422.39 kwa ajili ya ujenzi wa maabara za kisasa katika mikoa ya Dodoma na Mwanza, hatua inayolenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza gharama za upimaji wa sampuli.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema maabara zitakazojengwa katika mikoa hiyo zitaleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za viwango.
Amesema kuwa maabara zitakazojengwa mkoani Dodoma zitatumika kuhudumia mikoa ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora, huku maabara za Mwanza zikitumika kuhudumia mikoa sita ikiwemo Kagera, Mara, Geita, Shinyanga pamoja na Simiyu.
“Ujenzi wa maabara hizi utasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi, jambo litakaloboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika upimaji wa sampuli,” amesema Dkt. Katunzi.
Dkt. Katunzi amebainisha kuwa hadi sasa, TBS ina jumla ya maabara 12 zilizopata ithibati ya umahiri na vyeti vya kimataifa, hatua inayomaanisha kuwa majibu yanayotolewa na maabara hizo yanatambulika kimataifa.
Aidha, Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 12.9 kununua mashine za kisasa (state-of-the-art equipment) kwa ajili ya maabara hizo, zenye uwezo wa kutoa majibu kwa wakati sahihi na kwa usahihi mkubwa.
Baadhi ya Mashine za Kisasa zilizonunuliwa ni pamoja na Hydrostatic Pressure Test Machine, ambayo inapima mabomba ya maji, ikiwa na uwezo wa kupima mabomba kuanzia kipenyo cha inchi 0.5 (mm 12) hadi inchi 32 (mm 800), na inaweza kupima hadi sampuli 120 kwa wakati mmoja. Mashine hii inapatikana katika nchi tano pekee barani Afrika, ikiwemo Tanzania.
Mashine nyengine ni Automatic Conductor Resistance Tester ambayo upima waya (cables) za umeme wa aina zote zenye kipenyo hadi kufikia milimita 40 au milimita za mraba 1,200.
Pia mashine ya Solar Simulator, ambayo upima ubora wa paneli za sola bila kutegemea mwanga wa jua. Katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, mashine hii inapatikana Tanzania pekee, katika ofisi za TBS.
Dkt. Katunzi ameeleza kuwa TBS imetenga shilingi milioni 350 kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo na wa kati nchini, kwa kuwasaidia bidhaa zao kupata uthibitisho wa ubora.
Amesema kuwa huduma hiyo hutolewa kwa kuzingatia mahitaji ya kila halmashauri, na kwamba TBS itaendelea kushirikiana na watendaji wa halmashauri nchini kote ili kuwatambua wajasiriamali wenye bidhaa zenye uhitaji wa kuthibitishwa ubora lakini hawana uwezo wa kifedha.
“Lengo ni kuhakikisha bidhaa za wajasiriamali wa ndani zinatimiza viwango bora ili ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” ameongeza Dkt. Katunzi.
Dkt. Katunzi ametoa wito kwa wazalishaji na waingizaji wa bidhaa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia TBS, ili kuhakikisha bidhaa zinakuwa salama na zenye ubora unaokubalika.
Akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena ametoa wito kwa TBS kuendelea kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari kwa kuwaelimisha kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo viwango. Ameeleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza uelewa wa umma kupitia vyombo vya habari.