Wadau wa maendeleo, wasomi na wataalamu kutoka sekta binafsi na ya umma wamesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kupitia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2025, licha ya changamoto za kiuchumi za kimataifa.
Hata hivyo, wametaja kuwa sekta ya kilimo bado ni dhaifu kutokana na utegemezi wa mvua na ukosefu wa viwanda vya zana za kilimo.
Wameshauri kuongezwa kwa uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, huduma za kiuchumi, na ushiriki wa vijana katika kilimo.
Hoja hizo zimeibuliwa katika Kongamano la Uchumi Jumuishi lililofanyika wiki hii katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Kigoda cha Profesa cha Mwalimu Julius K. Nyerere, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).
Washiriki wamesisitiza umuhimu wa kujenga uchumi jumuishi unaogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Mwenyekiti wa kongamano hilo, Profesa Alexander Makulilo, amesema kuwa lengo kuu la kongamano hilo ni kuchochea mijadala juu ya ujenzi wa uchumi shirikishi na endelevu.
Ameeleza kuwa kongamano hilo limekuja wakati muafaka, muda mfupi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua rasmi Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 mnamo Julai 17, 2025. Profesa Makulilo amesisitiza kuwa utekelezaji wa dira hiyo unamhusu kila Mtanzania na unahitaji ushiriki wa pamoja.
Akielezea kuhusu maudhui ya Dira ya 2050, Ndugu Jordani Matonya amesema kuwa dira hiyo imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, usalama, amani na utulivu. Amesema kuwa dira hiyo ina nguzo kuu tatu: uchumi jumuishi na imara, maendeleo ya watu, na uhifadhi wa mazingira.
Amezitaja sekta za mageuzi zitakazowezesha utekelezaji wa dira hiyo kuwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji, utalii, viwanda na huduma za kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Bw. David Kafulila, ameeleza kuwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa bandari, barabara na majengo ya kisasa.
Amesisitiza kuwa sekta binafsi ni mhimili muhimu katika kufanikisha Dira ya 2050.
Washiriki wengine wa kongamano hilo wamesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi wote katika utekelezaji wa dira hiyo kupitia matumizi ya teknolojia, mabadiliko ya mitazamo, na mshikamano wa karibu baina ya sekta zote.