Na Meleka Kulwa – Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka wanaushirika wa mkoa huo kutumia kikamilifu fursa za miundombinu ya kisasa iliyowekwa na serikali, ikiwemo uwanja wa ndege wa kisasa, reli ya kisasa ya SGR na barabara ya mzunguko, ili kuongeza tija katika kusafirisha mazao na kukuza uchumi wa wanachama.
Akizungumza Septemba 19, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, wakati wa usajili wa washiriki wa kikao cha wadau wa ushirika, Mkuu Wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule amesema kuwa miradi hiyo mikubwa haipaswi kushangiliwa tu bali itumike kama chachu ya maendeleo ya kiuchumi.
“Kila fursa mnayoisikia mnatakiwa muitafsiri kama manufaa ya kiuchumi. Dodoma ndiyo mkoa pekee ulionufaika zaidi na miradi hii ya kimkakati. Hii si bahati mbaya, bali ni matokeo ya juhudi za serikali yetu kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Aidha, Bi. Rosemary senyamule amebainisha kuwa utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii ni sehemu ya kukuza uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi. Aliongeza kuwa vikao hivyo vina lengo la kutoa mrejesho kuhusu mafanikio ya serikali, kupokea maoni ya wananchi na kusikiliza changamoto zinazokabili vyama vya ushirika.
Amesema kuwa sekta ya ushirika ni nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania na kwamba vyama vingi vya ushirika vimeanza kuimarika kutokana na sera na taratibu mpya zilizowekwa na serikali.
“Nashukuru serikali yetu kupitia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameimarisha taratibu na sheria za vyama vya ushirika, jambo ambalo limewezesha sekta hii kuendelea kustawi,” alisisitiza.
Aidha, amewataka wanaushirika kutambua mchango wa miradi ya kimkakati katika kuongeza mapato, kupunguza gharama za uzalishaji na kupanua masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi.
Pia, Bi. Rosemary Senyamule amebainisha kuwa Mkoa wa Dodoma, hususan Jimbo la Dodoma Mjini, ndilo lililoshika mkia kitaifa kwa idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, huku Jimbo la Chamwino likiongoza kwa idadi kubwa ya wapiga kura kitaifa.
Amesema wakazi wengi wa Dodoma hutumia nguvu na muda wao kujiandikisha lakini hawajitokezi kupiga kura siku ya uchaguzi, hivyo akawahimiza wananchi wote waliojiandikisha—asilimia 94 ya wakazi wa Dodoma
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Dodoma (DOVECU), David Mwaka, alitoa rai kwa wanaushirika kutumia fursa ya kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo, akibainisha kuwa serikali ya Awamu ya Sita inawaunga mkono wakulima.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya UDOM SACCOS, Dkt. Leone Mujwahuzi, alisema wanaendelea kuimarisha jukwaa la maendeleo ya wanaushirika kila mwaka ili kujadili mafanikio, changamoto na kuweka misimamo ya pamoja kwa maendeleo ya baadaye.
Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, Joseph Meshack Chitinka, alisema zaidi ya vyama 100 vya ushirika mkoa wa Dodoma vimeshajiunga na mfumo wa MOVU, ambao umewezesha taarifa zote za wanaushirika kusomeka kupitia mtandao. Aliongeza kuwa wanaushirika wa Dodoma hurejesha kwa jamii kila mwaka kwa kutoa misaada kwa wenye uhitaji, ambapo mwaka huu walitoa msaada katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino.
Kikao hicho kiliwaleta pamoja viongozi wa vyama vya ushirika, wadau wa maendeleo na maafisa wa serikali, kikilenga kujadili mbinu za kuboresha sekta hiyo katika mkoa wa Dodoma.