

Wafanyabiashara 40 wa Soko la Mashine Tatu, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, waliopoteza bidhaa na mali zao kufuatia ajali ya moto, wamekabidhiwa hundi ya Shilingi milioni 120 kutoka kampuni ya Reliance Insurance kwa kushirikiana na Benki ya NMB, ikiwa ni fidia inayolenga kuwasaidia kurejesha mitaji na kuendeleza biashara zao, huku wafanyabiashara wengine wakihimizwa kujiunga na bima ili kujikinga na majanga ya aina hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo leo Septemba 18, 2025 katika soko la Mlandege, Kamishna wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware, amesema tukio hilo ni mfano halisi wa faida za kuwa na bima katika biashara, huku akiwataka wafanyabiashara kuendelea kutambua wajibu wao wa kulinda mali zao.
Dkt. Saqware ameeleza kuwa elimu ya bima ni muhimu sana, kwani mara nyingi wafanyabiashara wengi hujikuta kwenye shughuli za kila siku bila kuzingatia namna ya kujikinga na majanga yasiyotabirika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya bima ya Reliance Insurance, Ravi Shankar, amewashukuru wafanyabiashara wote kwa kujitokeza katika warsha hiyo na kupongeza mshikamano waliouonyesha baada ya wenzao kuathirika.
Shankar amesema Reliance Insurance itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wa Iringa, huku akiwataka kutokata tamaa bali kuendelea kuamini huduma za bima kama nguzo ya kulinda biashara.
Kwa niaba ya kampuni, Shankar amesisitiza kuwa bima siyo gharama bali ni uwekezaji wa usalama, akiwataka wafanyabiashara kuendeleza ushirikiano na kampuni za bima na benki.
Kwa upande wake Afisa biashara wa Mkoa wa Iringa, Asifiwe Mwakibete, ameishukuru Benki ya NMB na Reliance Insurance kwa mshikamano wao, akisema tukio hilo limewafungua macho wafanyabiashara wengi kuhusu umuhimu wa bima.
Asifiwe ameeleza kuwa mara nyingi wafanyabiashara hutambua thamani ya bima pale majanga yanapowapata, lakini ni vyema kuwa tayari mapema ili kupunguza madhara.
”Nawaomba viongozi wa taasisi za kifedha na bima kuendelea kutoa elimu endelevu, pia niwatake wafanyabiashara waliopokea fidia hii kuwa mabalozi wa kuhamasisha wengine kujiunga,” amesema Asifiwe
Rafael Ngulo, Mwenyekiti wa Umoja wa Masoko wa Manispaa ya Iringa, amesema tukio hilo limewafariji sana wafanyabiashara waliopoteza mali zao, kwani wengi walikuwa kwenye hali ngumu baada ya kuunguliwa bidhaa na mitaji.
Katika hatua nyingine Ngulo ameongeza kuwa mshikamano ulioonyeshwa na Benki ya NMB pamoja na Reliance Insurance ni jambo la kuigwa, na kwamba wafanyabiashara watandelea kushirikiana na taasisi hizo.
Aidha Mkuu wa Idara ya Bima kutoka Benki ya NMB, Martin Masawe amefafanua kuwa utaratibu wa madai kwa wafanyabiashara wa Iringa ulikuwa mwepesi na hauna usumbufu, jambo lililoleta imani kubwa kwa wateja.
”Niseme tu kwamba bima za biashara huanzia Shilingi 10,000 pekee na zinaweza kulipwa fidia ya hadi Shilingi 500,000, na hivyo kuwa nafuu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati,” amesema Masawe
Katika kulisisitiza suala hilo Masawe amekiri kuwa benki hiyo itaendelea kutoa elimu ya kifedha kwa wafanyabiashara, na pia kuhamasisha mikopo kwa ajili ya kuongeza mitaji na kukuza biashara zao.
Miongoni mwa wafanyabiashara waliopokea hundi, wameeleza kuwa fidia hiyo imewatoa kwenye hali ya hofu kwani mali zote ziliungua moto, na sasa wanaweza kuanza upya biashara kwa ujasiri.
”Sijui niseme nini lakini msaada huu wa fidia umenipa nguvu ya kurudi sokoni, na niwaombe wafanyabiashara wenzangu wasikate tamaa bali waendelee kuamini huduma za bima,” amesema Maria Ngoda Mfanyabiashara wa mali mbichi soko la Mlandege.
Wafanyabiashara hao kwa pamoja waliishukuru Reliance Insurance na NMB kwa msaada huo, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na kuhamasisha wenzao katika masoko yote ya Iringa.
Hafla hiyo imeacha somo kubwa kwa wafanyabiashara mkoani humo kuwa bima si hiyari bali ni nguzo muhimu ya maendeleo ya biasha ra na maisha ya kila siku.