NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Wananchi wamejitokeza kwa wingi katika Maonesho ya pili ya Afya ya Masaki (Masaki Health Expo) yaliyofanyika leo Septemba 21, 2025 katika mtaa wa Twiga 06, Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya taasisi na watoa huduma 20 wameshiriki kwa kutoa elimu na huduma mbalimbali za afya bure.
Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Masaki Wellspring Hub (MWH) yamehusisha huduma za lishe, tiba ya viungo (physiotherapy), afya ya akili, afya ya uzazi pamoja na afya ya kinywa na macho.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa MWH, Dkt. Yonazi Charles, amesema lengo la maonesho hayo ni kuelimisha jamii kuhusu mitindo bora ya maisha na kutoa huduma muhimu kwa kushirikiana na wadau wa afya.
“Muitikio umekuwa mkubwa. Wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata huduma mbalimbali, na tunahimiza kila mmoja kutumia fursa ya maonesho haya ambayo ni bure kushiriki,” amesema Dkt. Charles.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Kliniki za Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) katika Halmashauri ya Kinondoni, Dkt. Omary Mwangaza, amewataka wananchi kutumia maarifa waliyopata kubadili mitindo ya maisha ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.
“Magonjwa mengi yanachangiwa na mitindo ya maisha. Kila mmoja anatakiwa kuchukua hatua mapema kujali afya yake,” amesema na kuipongeza MWH kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza afya za wananchi kupitia elimu na huduma za bure.
Miongoni mwa watoa huduma walioshiriki, ONA Eye Care ilitoa huduma za uchunguzi wa macho, ambapo mwakilishi wake, Bi. Neema Elly, amewaonya wazazi kuhusu madhara ya watoto kutumia muda mwingi kwenye simu, televisheni na tablet.
“Matumizi ya vifaa hivyo muda mrefu husababisha changamoto kubwa za macho, hivyo ni vyema wazazi wakawa makini,” amesema.
Aidha, Maple Bloom School kupitia Mkurugenzi wake, Bi. Matilda Sizya, imeshiriki kwa kutoa elimu ya lishe bora kwa watoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 18, huku akibainisha changamoto kubwa ipo kwenye uelewa wa malezi na makuzi.
Wananchi waliohudhuria wameipongeza Shirika la MWH na wadau wake kwa kuandaa maonesho hayo waliyoyataja kuwa msaada mkubwa kwa jamii, kutokana na kupata huduma bora na ushauri kutoka kwa wataalamu bila malipo.