Na.Sophia Kingimali.
Katika maadhimisho ya Siku ya Amani Vijana kote nchini wametakiwa kutambua kwamba amani na usalama ni chachu ya maendeleo ya taifa hivyo wanapaswa kuvilinda na kujiepusha kuwa chanzo cha kuharibu amani hiyo.
Akizungumza Octoba,2025 Juma Rashid Ally, Afisa uwezeshaji kiuchumi kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar amewapongeza na kuwashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kulinda na kuimarisha amani ya nchi.
“Amani inaanza na kauli zetu tunazotumia kila siku. Vijana hawana budi kuelewa kwamba bila utulivu, hatuwezi kupiga hatua za maendeleo. Wao ndio uti wa mgongo wa taifa, hivyo wasikubali kutumiwa kuvunja mshikamano, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania ni taifa la mfano barani Afrika hivyo vijana wanapaswa kulinda amani kama njia mojawapo ya kuwaenzi waasisi wa taifa.
Pia Aliwahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi, wakichagua viongozi kwa amani na busara, bila kuruhusu tofauti za kisiasa kugawa jamii.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa wito wa pamoja kwa vijana wa Kitanzania kuapa kuilinda amani na usalama wa nchi, kuhakikisha mshikamano unabaki kuwa alama ya taifa hata wakati wa mabadiliko ya kisiasa.
Kwa upande wake barozi wa Amani ambae pia ni kijana Irene Ishengoma ameipongeza uwezeshaji wa vijana uliofanywa na serikali zote mbili katika kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo mbalimbali lakini kuhakikisha wanapata elimu ya ufundi unaowasaidia kuweza kujiajili.
“Tunapozungumzia amani ni pamoja na uchumi kijana anapokuwa vizuri kiuchumi awezi kufikilia kupotoka na kutumika kuwa kichocheo cha kuvunja amani kiukweli serikali zetu zimejitahidi sana kuhakikisha sisi vijana tunakuwa kwenye mazingira mazuri”,Amesema.
Naye,Silvia Mkomwa ambae ni barozi wa amani amesema uwepo wa majukwaa kama hayo ya amani yanachagiza kujadili jinsi gani vijana wanashiriki katika ujenzi wa amani nchini ili kuofanya nchi kuendelea kubaki kuwa nchi ya mfano katika ulinzi wa amani Afrika.
Tukiangalia Tanzania tumekuwa tukionekana kama nchi ya mfano wa amani ya kuiga hivyo kama vijana tutaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa ya mfano katika kulinda Amani”,Amesema.