Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mapato na Uwekezaji, Bw. Leonard Msafiri, akieleza mchango wa sekta ya ardhi katika mapato yasiyo ya kodi, wakati wa Kikao cha Maafisa Masuuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
………
Eleuteri Mangi, WANMM, Dodoma
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni miongoni mwa Wizara na taasisi za Serikali zinazokusanya mapato yasiyo ya kodi kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ambayo huwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Akizungumza jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mapato na Uwekezaji, Bw. Leonard Msafiri amesema Wizara hiyo inatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato kwa kutumia control number jumuishi ambazo zinatolewa kupitia mifumo mbalimbali inayosimamiwa na Wizara ikiwemo Molis, Ilmis na e-Ardhi kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na serikali.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara hiyo imejipanga kukusanya Shilingi bilioni 290 na ilipewa jukumu la kukusanya kodi tangu mwaka 1996 kwa sasa inakusanya Shilingi bilioni 156 tofauti na hapo awali ambapo ilianza kukusanya Shilingi bilioni 48.
Ili kufikia malengo hayo, Wizara imejipanga kujenga uwezo katika vituo vya ukusanyaji mapato katika mikoa 26 na Halmashauri 185 nchini hatua inayosaidia kuongeza wigo wa kuwafikia walipa kodi wengi zaidi katika sekta ya ardhi ikiwemo urasimishaji wa maeneo yataongeza ufanisi katika kukusanya maduhuli ya serikali.
Akifunga Kikao cha Maafisa Masuuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayesimamia Uchumi, Bw. Elijah Mwandumbya amewasihi Maafisa Masuuli kuendelea kutekeleza majukumu yao ya ukusanyaji wa mapato kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo na kuwasilisha mapato hayo katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa wakati.