Na Mwandishi Wetu
MAHOJIANO ya wanafunzi na wataalam wa barabara yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Usalama barabarani la Amend kwa msaada kutoka Cotswold Foundation yamefanyika mkoani Dar es Salaam yakilenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu usalama barabarani na kushirikisha wataalamu wanaohusika na usanifu, ujenzi na ukarabati wa barabara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo kuhusu mahojiano hayo yaliyofanyika Shule ya Msingi Tegeta amesema yamewakutanisha wanafunzi wa Shule za Msingi Pius Msekwa, Kunduchi, na Tegeta, zote ziko kando ya Barabara ya Silver.
Ambapo amesema wanatazamiwa kunufaika na Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2). Kupitia majadiliano na wanafunzi hao, mradi ulilenga kukusanya maoni na uzoefu wao kuhusu safari zao za kwenda na kurudi shuleni.
“Mpango huu unaangazia umuhimu wa kushughulikia mahitaji ya watumiaji wa barabara walio hatarini ambao wako katika hatari kubwa.Mjadala huui ni sehemu ya mpango mpana zaidi wa kukuza mtazamo wa ‘kuzingatia watu’ au ‘kuzingatia mtoto’ katika ujenzi wa barabara.
“Na kuacha mtindo wa kawaida wa kuyapa kipaumbele magari. Mradi wa DMDP 2, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa zaidi ya dola milioni 330, unatazamiwa kuboresha takriban kilomita 260 za barabara kati ya 2025 na 2030.
“Lengo letu ni kuanzisha jukwaa ambalo watoto wanaweza kubadilishana uzoefu na mitazamo yao na viongozi na wahandisi wanaohusika katika miradi ya barabara,” alisema Simon Kalolo, Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania.
“Kwa kujumuisha mchango wa watoto katika mchakato wa kubuni, tunaweza kujenga barabara ambazo ni salama na zinazofaa zaidi watembea kwa miguu na watu wenye mahityaji maalumu.”
Ameongeza mpango huo unaungwa mkono na serikali ikiwemo TARURA na Benki ya Dunia, ambao wana nia ya kusimamia mahusiano ya umma kwa ufanisi. Kuwaleta watoto pamoja na maafisa wa mradi na wahandisi hutoa fursa ya ushiriki mzuri wa jamii.
“Ikiwa tutatetea kwa mafanikio ujenzi wa barabara inayolenga watoto, tunaweza kusaidia kuzuia vifo na majeraha mengi miongoni mwa watoto wanaotembea kwa miguu,” Simon Kalolo.
Pia amesema Amend inalenga kutumia vyombo vya habari kuongeza zaidi ufahamu wa usalama barabarani unaozingatia watoto miongoni mwa watunga sera, wataalamu wanaohusika na hatua zote za miradi ya barabarara na umma kwa ujumla.
“Lengo letu ni kuanzisha jukwaa ambalo watoto wanaweza kueleza changamoto na mitazamo yao ya usalama barabarani na viongozi na wahandisi wanaohusika katika miradi ya barabara,” amesema Kalolo.
Kwa upande wake Agatha Tembo kutoka DMDP-KMC, amesema ushirikiano baina ya wadau wote wa usalama barabarani ni muhimu katika kusaidia kuepusha ajali. Wajenzi wakiweka vibao vya mbao wakati wa ujenzi watoto au wazazi wasivichukue kwenda kugeuza kuni majumbani.
Wakati huo huo Jacinta Toke kutoka NIMETA CONSULT,Environment amesema ni vema jamii waelimishwe kwamba ni jukumu letu sote kutunza miundombinu ya barabara.“Tusichafue mazingira, mitaro ikaziba na maji yakafurika barabarani. “
Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Msingi Kunduchi Prosper Lyimo amesema walimu wawe wanakutana na wanafunzi asubuhi na baada ya masomo ili wawakumbushe hatari zinazoweza kutokea wakati wa ujenzi na wawahimize kuwa makini.