Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana ametoa rai kwa jeshi la polisi na waandishi wa habari kuzingatia maadili, miiko, sheria na taratibu katika kuelekea kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa Leo Jumatatu Septemba 22, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa jeshi la polisi na waandishi wa habari kuhusu haki za binadamu na wajibu wakati wa zoezi la uchaguzi mkuu.
Balandya amesema kwa pamoja jeshi hilo na wanahabari wanawajibu wa kulinda amani na kuhabarisha umma juu ya mwenendo wa uchaguzi kabla, wakati na baada ya uchaguzi katika kuelekea kuwapata viongozi watakao ongoza nchi ya Tanzania kwa amani.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Msataafu Mathew P. Mwaimu Bi. Saumu Mgeni ambaye ni Afisa Uchunguzi -Sheria amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa jeshi la polisi na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria wakati wa uchaguzi.
Amesema jeshi hilo lina wajibu wa kusaidia kuzingatia haki na misingi hiyo wakati wote kwa kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima sanjari na kuhakikisha wanalinda uhuru wa haki na amani.
Mafunzo hayo yanatolewa katika Mikoa 14 ya Tanzania Bara na mikoa mitano kwa upande wa Visiwani ambapo kwa upande wa mkoa wa Mwanza mafunzo yanawakutanisha washiriki 60 (Jeshi la Polisi 40 na Waandishi wa Habari 20)