
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam leo, Jumatatu Septemba 22.2025 imetoa majibu ya maombi yaliyowasilishwa Mahakamani hapo na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu kuhusiana na kuomba Mahakama iruhusu urushaji mubashara (LIVE streaming) kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili, inayoendelea Mahakamani hapo
Inaelezwa kuwa, mshtakiwa Tundu Lissu aliwasilisha maombi hayo Mahakamani hapo kupitia barua aliyomwandikia Msajili wa Mahakama, na pale alipoona maombi hayo yanakawia kujibiwa aliyawasilisha kwa jopo la Majaji watatu (3) wanaosikiliza kesi hiyo, ambao waliahidi kufuatilia na kutolea muongozo, ambao leo umetolewa rasmi
Akisoma maelezo hayo, kwa niaba ya wenzake Jaji Danstan Ndunguru amesema maelezo au muongozo wa hoja hiyo limejikita katika kanuni za msingi za usikilizwaji wa mashauri ya uwazi, lakini pia lengo la mtuhumiwa ni kwamba umma ufahamu kinachoendelea Mahakamani
Mahakama imesema inatambua wazi na mara zote inasimamia msingi wa kwamba haki sio tu itendeke bali ionekane inatendeka, kwa muktadha huo Mahakama imeangalia kanuni, taratibu na sheria zinasemaje kuhusu jambo hilo
Katika maelezo yake, Mahakama imesema mashahuri yote ya jinai yatafanywa katika Mahakama ya wazi kama inavyofanyika sasa Mahakamani hapo kwenye kesi hiyo, lakini kwa hapa Tanzania hakuna kanuni zozote zinazotoa maelezo ya kurushwa mubashara (live streaming)
Mahakama imesema, kwa muktadha wa shauri hilo, Mahakama inatambua kuwa kuna mashahidi wa siri, na kwamba inaeleweka kuwa pindi shahidi mmoja anapokuwa anatoa ushahidi wake Mahakamani, shahidi mwingine hatakiwi kuwepo kwenye chumba cha Mahakama, sasa endapo kesi hiyo itarushwa mubashara Mahakama haitaweza kudhibiti mashahidi wengine wasifuatilie kinachoendelea Mahakamani kwakuwa wanaweza kufuatilia matango mubashara wakiwa popote pale
Hata hivyo, kutokana na sababu hiyo na nyingineyo zilizoelezwa na Mahakama, Mahakama imeona haitafaa kesi hiyo kurushwa mubashara (live streaming), lakini kesi hiyo inaendelea kusikilizwa kwa uwazi na waandishi wa habari wanaruhusiwa kuendelea kufuatilia mwenendo wa kesi.