Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limepewa tuzo kwa kuwa kufadhili ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya Maonesho ya Kimataifa ya Nane ya Teknolojia ya Madini Mkoani Geita yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Tuzo hiyo imetolewa leo tarehe 22 Septemba,2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa na kupokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Ndugu Deusdedith Magala kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt.Venance Mwasse mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mha. Yahya Samamba.
Maonesho haya yamefunguliwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo pia alitembelea Kijiji cha STAMICO na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika katika kusaidia Wachimbaji Wadogo.
Alilipongeza Shirika kwa uwekezaji mkubwa wa mitambo ya kisasa ya uchorongaji wenye uwezo wa kuchoronga zaidi ya mita 3000 sawa sawa na KM3.
Mhe.Waziri Mkuu alipongeza namna Shirika linavyojali na kuwasaidia wachimbaji wadogo ambapo sasa wameanza kunufaika na rasilimali madini.
Maonesho haya ya Madini yenye kaulimbiu “Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia sahihi na Uongozi Bora, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025” yameanza tarehe 18 Septemba 2025 na yatahitimishwa tarehe 28 Septemba, 2025.