
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imekionya chama cha ACT-Wazalendo kutoendelea kuwatambulisha Luhaga Mpina na Fatma Ferej kuwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani leo Septemba 22, imesema Chama cha ACT-Wazalendo hakina wagombea husika kutokana na pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Taarifa hii ya INEC inakuja kufuatia taarifa iliyotolewa na ACT-Wazalendo kubainisha uwepo wa mkutano wa uzinduzi wa ilani ya uchaguzi na kampeni za ubunge Jimbo la Segerea. Tume imesema kuwa taarifa zilizodai kuwa Luhaga Joelson Mpina na Fatma Abdulhabib Ferej ni wagombea wa nafasi hizo si za kweli.
INEC imesisitiza kuwa ACT-Wazalendo kilitaarifiwa kwa barua rasmi kuhusu uamuzi huo tangu Septemba 15, 2025 na kuikumbusha kutii masharti ya Kanuni ya Uchaguzi yanayohusu uendeshaji wa kampeni.