Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali (Public Bar Association – PBA), Wakili Ado Mwasongwe akizungumza na waandishi wa habari jijini Da es Salaam leo Septemba 23, 2025.
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
CHAMA cha Mawakili wa Serikali (Public Bar Association – PBA) kimetoa tamko rasmi kupinga maazimio ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society – TLS) kuhusiana na tukio la Septemba 15, 2025, kikisisitiza kuwa maamuzi ya TLS yanakiuka Katiba na sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Da es Salaam leo Septemba 23, 2025, Mwenyekiti wa PBA, Wakili Ado Mwasongwe, amesema chama hicho kimeona ni muhimu kutoa ufafanuzi wa kisheria na kikatiba ili kulinda maslahi ya taifa na haki za wananchi.
“TLS ni chama cha kitaaluma kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria. Kila wakili aliyeandikishwa ni mwanachama wake, wakiwemo mawakili wa Serikali na hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ni lazima tamko lolote la TLS liwe na weledi wa kisheria, si msukumo wa kiharakati,” amesema Wakili Mwasongwe.
PBA imeonya kuwa hatua ya TLS kuzuia wanachama wake kutoa msaada wa kisheria ni kinyume cha Katiba na Legal Aid Act, na inaleta hatari ya kunyima wananchi maskini haki ya msingi ya kupata msaada wa kisheria.
“Huduma za msaada wa kisheria siyo hiari wala hisani. Ni jukumu la kisheria lililowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria na kila wakili anapaswa kutoa huduma hiyo kwa wote, wenye uwezo na wasio na uwezo,” ameongeza.
Ameeleza kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza usawa mbele ya sheria (Ibara ya 13) na wajibu wa kila mtu kutii Katiba na sheria (Ibara ya 26).
“Hivyo, hatua ya TLS ya kuwanyima wananchi wa kipato cha chini msaada wa kisheria ni kitendo cha ubaguzi na kinyume cha Katiba.” Amesema
Aidha, Wakili Mwasongwe amewakumbusha kuwa nidhamu ya mawakili ipo chini ya Kamati ya Nidhamu ya Mawakili inayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, hivyo si jukumu la TLS pekee.
“Tunashauri kwa heshima viongozi wa TLS kuzingatia wajibu wao wa kisheria na kitaaluma, na waache mara moja kuchagua sheria za kutii kulingana na maslahi yao binafsi. Wanapaswa kutii sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesisitiza Wakili Mwasongwe.
PBA imesema itaendelea kutetea utawala wa sheria, kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha wananchi wote, hususan wenye kipato cha chini, wanapata huduma za kisheria bila ubaguzi.