*Amshukuru kwa ushirikiano, kujituma,uzalendo wake kwa wakati wote wakifanyakazi pamoja.
*Azungumzia pia maendeleo yaliyopatikana Ruangwa katika miaka mitano iliyopita
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Ruangwa
MGONBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewashukuru wananchi wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kwa kumchagua Kassim Majaliwa kuwa mbunge wao kwa kipindi cha miaka 15.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu,Mgombea urais Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kumzungumzia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amefanya kazi ya Waziri Mkuu kwa miaka 10.
“Yaliyosemwa hapa kwamba yametekelezwa ni kazi yake kwani ndiye msimamizi wa shughuli za serikali. Wanaruangwa mmefanyakazi nzuri sana kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana vizuri na Mbunge wenu.
Hata hivyo amesema kwa kushirikiana na Waziri Mkuu wamefanikiwa kutekeleza miradi ya maendeleo na kwamba Serikali itaendelea kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa maendeleo ni jambo ambalo linafanyika kila siku.
“Wakandarasi wamefanyazi nzuri kutekeleza miradi ya maendeleo yote iliyokuja kwa sababu tumewapa nafasi wakandarasi wanendelee na kazi yao,” amesema Dk.Samia na kuwapongeza wananchi kwa kutoa maeneo kupisha miradi ya maendeleo.
“Ninapowashukuru ninyi ninamshukuru sana yeye mwenyewe Kassim Majaliwa kwa ushirikiano wake, kujituma kwake, uzalendo wake, wakati wote tumefanyakazi pamoja.
Aliongeza: “Lakini pia wakati wote aliokuwa mbunge wa jimbo hili, yaliyosemwa ni hakika nguvu yake, msukumo wake na ndiyo maana Ruangwa ya leo imepiga hatua.”
Pamoja na hayo Dk.Samia ametoa ahadi kwa wananchi wa jimbo hilo kuwa anatambua na kuthamini mchango wa Waziri Mkuu Majaliwa, hivyo ataendelea kuwa msaidizi muhimu katika serikali.
Amefafanua katika jimbo hilo kwenye sekta za afya, elimu, maji, umeme, kilimo, barabara yote yamefanyika.”Magendeleo ni hatua hivyo niwaahidi wananchi serikali itaendelea kutimiza wajibu wake kwani bado kuna maeneo ya kipaumbele ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi.
“Serikali inafahamu mahitaji ya wananchi yanaongezeka kwa sababu hiyo itaendelea kufanyakazi sekta zote za maendeleo ya jamii ili wilaya hiyo ipige hatua zaidi.Tulianza kuna vituo vya afya nane vipya vimejengwa.
“Nikawa namuuliza Waziri Mkuu mnakata ngapi? Akaniambia zipo kata zaidi ya 20, nielewa kwamba kazi bado ipo.Bado tutakuja kujenga vituo vya afya, bado tutakuja kujenga zahanati, shule za msingi na sekondari tutahakikisha miradi yote ya maji inayotekelezwa ina kamilika kila mwanaruangwa apate maji safi na salama.”
Pia amesema serikali inakwenda kukamilisha kuunganisha umeme katika vitongoji ili nishati hiyo ikatumike nyumbani, kulinda usalama na shughuli za uzalishaji.
“Serikali imetanguliza nishati ya kutosha kwa lengo la kuanzisha kongani za viwanda kwa sababu sekta ya hiyo inakuwa kwa kasi wilayani Ruangwa.Umeme utarahisisha maendeleo ya viwanda na kukuza uzalishaji.”
Kuhusu mkakati wa kudhibiti wanyamapori waharibifu wanaovamia mashamba ya wananchi amewaahidi Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti wanyama waharibifu .
“Niwaahidi kwamba kazi ipo na tunakuja kuifanya. Naelewa katika maeneo ya vijiji vya Madangilo, Magawa, Lugombe, Mbwemkulu kuna tatizo la wanyama kufanya uharibifu kwenye mashamba.
“Hili ninalielewa vyema na mkiwakuta wale wanyama waambieni dawa yao ipo jikoni. Wanyama tunawapenda lakini lazima tuwalinde, tuwazuie wabaki kwenye hifadhi zao.”