Mganga Mkuu wa Mkoa Geita (RMO), Dkt. Omari Sukari, ameipongeza Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwa kushiriki katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini – Geita na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu, likiwemo la kukinga amana za wateja wa benki na taasisi za fedha.
“Napenda kuwapongeza kwa kushiriki katika maonesho haya na kupata nafasi ya kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu yenu. Hata mimi nina amana zangu kwenye benki kadhaa, sasa najua kabisa kwamba fedha zangu ziko salama hata kukitokea shida ya benki kufa,” amesema Dkt. Sukari.
Amesema ni muhimu wananchi kuendelea kupata huduma za kibenki, ikiwemo kufungua akaunti za benki wakijua kwamba pesa yao iko salama kwa sababu kuna DIB ambayo inakinga amana zao.
Aidha, alifurahia kusikia kwamba DIB itakuwa na jukumu la kupunguza hasara katika benki au taasisi ya fedha inayopitia changamoto ili kuiokoa irudi katika utendaji wa kawaida badala ya kusubiri hadi benki ife.
Ütaratibu huu ni mzuri sana wa kuokoa benki inapopitia changamoto ili irejee na kuendelea kufanya kazi kama kawaida, badala ya kusubiri hadi benki inapokufa,” alieleza RMO baada ya kupata maelezo kuhusu majukumu ya DIB.
Mapema Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita alipokelewa na maafisa wa DIB na kuelezwa majukumu ya DIB pamoja na jinsi taasisi hiyo inavyotoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake na kuwahakikishia kwamba amana zao katika benki zinakingwa na bodi hiyo.