Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mpango wa TACTICS imetoa kiasi cha sh. bilioni 19.8 bila jumuisho la kodi ya ongezeko la thamani (VAT)kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu mikubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa soko la kisasa la Mnarani na barabara mbili zenye urefu wa jumla ya kilomita 4.8.
Barabara zitakazojengwa ni barabara ya Tughe–Anglican yenye urefu wa kilomita 1.1 na barabara ya Picha ya Ndege–Hospitali ya Lulanzi–NDC yenye urefu wa kilomita 3.7.
Mkataba wa utekelezaji wa miradi hiyo umesainiwa septemba 25,2025 kati ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa na Mkandarasi M/s Dimetoclasa Real Hope Limited, katika hafla iliyoshuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Kunenge alisema Serikali inaleta miradi hiyo muhimu kwa wananchi wa Kibaha kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuinua hali ya uchumi wa wananchi, hususan wenye kipato cha chini.
“Tunafahamu kuwa wananchi wanahitaji huduma bora katika masoko, na ndiyo maana Serikali imeanzisha mradi huu, lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata mazingira mazuri ya kufanyia biashara kwa ubora unaostahili,” alisema Kunenge.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara watakaotumia soko hilo kushiriki kugharamia uendeshaji wake, akisisitiza kuwa fedha zilizotumika ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na hivyo zinapaswa kurejeshwa.
Kunenge pia alisema hadhi ya Manispaa ya Kibaha inapaswa kuendana na huduma zinazotolewa kwa wananchi, hivyo miradi hiyo ni sehemu ya kuboresha taswira ya mji na maisha ya wakazi wake.
Katika hatua nyingine, alimuelekeza mkandarasi kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Nafahamu uwezo wenu uko vizuri, mmehakikishiwa kuwa fedha zipo, hivyo sitarajii kuona changamoto yoyote, ninataka mradi huu ukamilike ndani ya muda uliopangwa kama ilivyoelekezwa kwenye mkataba,” alieleza Kunenge.
Kwa upande wake, Mhandisi Emmanuel Manyanga, Muwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA ambae pia ni Katibu Msaidizi wa Mradi wa TACTICS, alisema lengo kuu la mradi huo ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji na kuwezesha Halmashauri kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi.
Alisema kazi zitakazofanyika kupitia mkataba huo ni pamoja na:Ujenzi wa barabara ya Tughe–Anglican (km 1.1),Ujenzi wa barabara ya Picha ya Ndege–Hospitali ya Lulanzi–NDC (km 3.7),Ujenzi wa soko la kisasa la Mnarani na Uboreshaji wa bustani ya mapumziko ya mji.
Mradi huu kwa Manispaa ya Kibaha utaongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuboresha hali za biashara katika maeneo husika na hivyo kuchangia maendeleo ya muda mrefu ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Alibainisha utafungua milango ya usafiri na usafirishaji na kupendezesha Manispaa hiyo inayokua kwa kasi na kuipa hadhi inayostahili.
Utekelezaji wa mkataba huo unatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 1, 2025 na kukamilika Desemba 12, 2026.