Mgeni Rasmi, Eng. Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, aki ata Utepe kuashiria uzinduzi wa kituo hicho kulia kwake mwenye kiremba cheupe ni Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania.
Dar es Salaam, 24 Sept, 2025
PUMA Energy Tanzania leo imezindua kituo chake cha kwanza cha rejareja cha Gesi Asilia iliyoshindikizwa (CNG) kilichopo Tangi Bovu, Barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam.
Uwekezaji huu wa kihistoria unaweka kampuni katika mstari wa mbele wa suluhu za kisasa za nishati nchini.
Hafla ilihudhuriwa na Mgeni Rasmi, Eng. Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, pamoja na Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Carol Mundle, Kaimu Balozi, Ubalozi wa Canada, na viongozi wa Puma Energy.
Kituo hiki kipya kina uwezo wa kuzalisha gesi milioni moja za futi za ujazo kwa siku, na kinaweza kuhudumia magari madogo, makubwa na bajaji.
Kina mashine mbili za kisasa zenye uwezo wa kuhudumia magari 50 kwa saa, compressor kutoka Canada yenye nguvu ya 250 HP (1,200 Sm³/hr), na hifadhi ya gesi ya lita 4,000 inayohakikisha huduma bila kukatika hata wakati wa mahitaji makubwa.
Wateja pia watanufaika na mfumo wa ukaguzi wa ubora wa gesi unaohakikisha usalama na ufanisi.
Kituo hiki cha Bagamoyo Road pia ni cha kisasa zaidi kwa kuwa kinatoa huduma za CNG pamoja na petroli, dizeli, LPG, vilainishi na duka dogo, na hivyo kuwa kituo cha huduma kamili kwa madereva na wafanyabiashara.
Bi. Fatma M. Abdallah alisema:
“Uzinduzi wa kituo hiki cha CNG ni hatua mpya kwa Puma Energy nchini Tanzania. Tuna furaha kuanzisha miundombinu ya kisasa inayopunguza uzalishaji wa hewa ya kaboni na kutoa huduma ya uhakika kwa wateja.
Muhimu zaidi, huu ni mwanzo—tuko tayari kufungua vituo zaidi kabla ya mwisho wa mwaka huu.”
Kwa upande wake, Bw. Emmanuel G. Bakilana, Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Masuala ya Kampuni, aliongeza:
“Wateja wetu wanaweza kuitegemea Puma kwa usalama, ubora na upatikanaji wa uhakika. Kituo hiki kinaonyesha uwekezaji wetu katika miundombinu ya kisasa na nafasi yetu kama kinara wa suluhu rafiki za usafirishaji.”