Mgombea Ubunge jimbo la Ngorongoro CCM, Yaniki Ndoinyo akizungumza katika mkutano wa kampeni hizo wilayani Ngorongoro.
…………
Happy Lazaro, Manyara
Wagombea Ubunge na udiwani wa Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Ngorongoro wameeleza dhamira yao ya kupigania ongezeko la bajeti ya maendeleo ya Halmashauri ya wilaya hiyo, kutoka Shilingi bilioni 88 ya sasa hadi kufikia Shilingi bilioni 200, ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi.
Katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika kata za Arashi na Piyaya, wagombea hao wameahidi kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, elimu, na kupunguza migogoro ya ardhi.
Mgombea ubunge CCM ,Yaniki Ndoinyo amesema kuwa, atahakikisha anafanya mabadiliko makubwa katika jimbo hilo huku akitatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wake lengo likiwa ni kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Kwa upande wake, Mgombea udiwani wa kata ya Arashi, amesema ukosefu wa maeneo ya malisho umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa jamii ya wafugaji, na kulazimu hatua za haraka kuchukuliwa.
Kwa upande wake Mgombea udiwani,CCM Methew Siloma amesema kuwa ,wakiwa kama madiwani kwa pamoja watashirikiana na mbunge kuhakikisha kunakuwepo na eneo la malisho kwa ajili ya wafugaji kwani imekuwa ni changamoto ya muda mrefu.
Katika mkutano huo, Kiongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai, Bw. Konini Martin, ameungana na wananchi kuitaka serikali kuzingatia changamoto zinazowakabili wafugaji, huku akieleza matumaini ya jamii hiyo kwa viongozi wa CCM.
Wagombea hao wanatarajiwa kuendelea na kampeni katika kata nyingine za wilaya ya Ngorongoro huku wakiahidi kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.